BAADHI ya timu zilizowahi kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ndizo zinashika nafasi nne za kwanza katika Ligi ya Championship inayoendelea hadi sasa.
Timu hizo ndizo zinazotamba katika ligi hiyo kwani zinachuana vikali kuwania nafasi mbili za kwanza ili kupata nafasi ya kufuzu moja kwa moja kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2025/2026.
Kwa mujibu wa kanuni, wakati timu mbili za kwanza zikipanda moja kwa moja kucheza Ligi Kuu, timu mbili zinazoshika nafasi ya tatu na nne, zitacheza mechi za mtoano ili kujaribu kupata nafasi hiyo.
Yaani, timu hizo mbili za Ligi ya Championship zinacheza na timu mbili kutoka katika Ligi Kuu zilizomaliza katika nafasi ya 13 na 14, ambazo zikipata ushindi wa jumla katika mechi zake za nyumbani na ugenini zinabaki katika Ligi Kuu Bara.
Na endapo timu hizo kutoka Ligi ya Championship zitapata ushindi wa jumla katika mechi zao za mtoano dhidi ya timu za Ligi Kuu, timu hizo au mojawapo zitafuzu kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ligi ya Champioship ya msimu huu inaendelea na imefikia patamu na timu zilizowahi kushiriki Ligi Kuu kwa nyakati tofauti, ndizo zinaongoza mbio hizo hadi sasa.

Bila shaka timu zimewahi kwa nyakati tofauti kushiriki ligi hiyo, hivyo zimenogewa sasa zinataka kuchonga
mzinga, hivyo zinachuana vikali kutaka kurejea tena katika ligi hiyo. Ligi Kuu Tazania Bara inashirikisha jumla ya timu 16, kama ilivyo kwa Ligi ya Championship, ina ushindani mkali na ina zawadi nono, hivyo kila timu inataka
kufanya kweli.
Pia, ukiondoa suala la zawadi nono, timu zinachuana vikali kuwania uwakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa. Kwa upande wa Championship, timu za Mtibwa Sugar, Mbeya City, Stand United na Geita Gold zipo katika mchuano mkali zikishikilia nafasi nne za kwanza kuusaka uongozi wa ligi hiyo.
Kwa sasa timu ya Mtibwa Sugar ndiyo kinara wa ligi hiyo kwa muda mrefu, ikisaka ubingwa wa Championship ili iweze kumaliza katika nafasi ya kwanza. Mtibwa Sugar na Geita Gold msimu uliopita zilicheza Ligi Kuu, hivyo zenyewe zinajua utamu na uchungu wa ligi hiyo.

Stand United ya Shinyanga nayo iliwahi kushiriki Ligi Kuu misimu ya nyuma, hivyo nayo inataka kurejea tena katika ligi hiyo inayoshika nafasi ya sita katika viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pamoja na kushika nafasi ya kwanza katika ligi, timu ya Mtibwa Sugar ilifungwa na Mbeya City katika mchezo wa pili, hivyo hiyo inaonesha jinsi gani mchuano ulivyo mkali.
Tunaweza kusema kuwa kichapo kutoka kwa Azam FC ndio kiliishusha Geita Gold na Azam pia, ikamaliza Ligi Kuu, ikiwa ya pili na kupata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika msimu uliopita. Mbali na hizo, timu zingine zilizopo katika nafasi hiyo ya timu 10 bora za kwanza ni TMA, Mbeya Kwanza, Bigman, Songea United, Polisi Tanzania na Mbuni.
Zinazozofuatia ni pamoja na Green Warriors, Kiluvya, Cosmopolitan, African Sports, Transit Camp na Biashara United. Timu hizo zote zimeshacheza mechi kadhaa, lakini baadhi zimeonesha ushindani mkali wa kuwania
ubingwa huo wa Championship au kupanda daraja.
Karibu kila timu imebakisha mechi sita, lakini ushindani ni mkali katika mbio za ubingwa na kupanda daraja. Mbeya City iliyopo katika nafasi ya pili nyuma ya Mtibwa Sugar, imeonesha makali yake kwa kuifunga Azam FC bao 1-0 hivi karibuni katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
Mbeya City imepitwa na Mtibwa Sugar kwa pointi tano hadi sasa, lakini imeonesha makali kwa kila timu inayokutana nayo. Timu hiyo imewahi kuvuma katika Ligi Kuu Tanzania Bara na wengi wanashangaa imeshukaje. Vile vile, kwa Mtibwa Sugar ambayo iliwahi kuwa bingwa wa Ligi Kuu ya Muungano, imeacha maswali mengi kwa wadau ilivyoshuka daraja msimu uliopita.

Wafungaji wanaoongoza kwa kupachika mabao katika ligi hiyo ni Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar aliyefunga
mabao 15 pamoja na Andrew Simchimba.
Anayefuatia kwa ufungaji ni Abdulaziz Shahame wa TMA mwenye mabao 13, anayefuata kwa ufungaji ni Naku James wa Mbuni FC mwenye mabao 11, wenye mabao nane kila moja ni Yusuf Mhilu wa Geita Gold, Boniphace Maganga wa Mbeya Kwanza na William Thobias wa Mbeya City.
Wenye mabao saba kila mmoja ni Andrew Chamungu wa Songea United na Anuary Jabir wa Mtibwa Sugar. Ni matarajio ya wadau wengi wa michezo, hasa kandanda kuwa mchuano mkali utaendelea hadi mwisho wa ligi hiyo na kutoa bingwa wa kweli kweli, ambaye ataonesha ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
0 Comments