Wasira aonya rushwa wagombea CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina taarifa baadhi ya wanachama wanaotaka ubunge wameanza kukiuka maadili kwa kutoa rushwa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amebainisha hayo alipozungumza na wanachama wa CCM na wananchi katika kikao cha ndani wilayani Ngara mkoani Kagera.

Wasira amekumbusha wanaotaka ubunge na wabunge waliopo wazingatie maadili na akaonya iwapo wana CCM wakichagua watu kwa sababu ya fedha, watakuwa wamewachagua kwa makosa.

Ametoa rai kwa wajumbe wa CCM watakaopiga kura kuchagua mgombea mmoja kati ya watatu na wapige kura kwa uhuru bila kupewa fedha na wataka ubunge.

“Huko nyuma hapa Ngara waliokuwa wanapiga kura ni wajumbe 700, lakini kwa sasa ni zaidi ya 10,000 ni wengi maana sasa hivi mabalozi wote wanapiga kura, kwenye kamati zenu za watu wanne kote huko wanapiga kura,” alisema Wasira.

Wasira alisema moja ya kazi yake ni kusimamia maadili hususani kwa wanaotaka ubunge na akasema wapo wanaonyemelea na wanafanya hivyo kwa kuvunja maadili.

“Wanaotaka ubunge baadhi yao nina habari zao wameanza kuvuruga maadili wanataka muwapigie kura kwa hela wanazowapa na Biblia inasema rushwa inapofusha… maana yake ni kwamba ukiona mtu anasambaza hela lazima ujiulize kwani hiyo imekuwa huduma?” alisema.

Aliongeza: “Na hili nalisema kwa wagombea wapya na wabunge waliopo, tunachunguza tunajua mwenendo huo, sasa nawaambia acheni kupofusha wajumbe na ninyi wajumbe na mabalozi wa nyumba kumi mtupe heshima ya kutuletea watu wazuri, ndio wajibu wenu”.

Wasira alisema vyama vingi vya siasa vilivyofanikisha kupatikana uhuru Afrika vimekufa lakini CCM imeendelea kuwepo kwa sababu imejikita na mizizi yake inaanzia chini, kila nyumba 10 kuna kiongozi wa nyumba na ana kamati.

“Kama chama hichi kingekuwa kinashikiliwa na sisi huku juu tungeweza kufikiria kipo kumbe hakipo, ndivyo ilivyotokea kwa KANU (chama kilichopigania uhuru Kenya), chama kilicholeta uhuru wa Kenya hakipo, Zambia hakipo, Uganda hakipo, lakini chama kilicholeta uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) na mapinduzi ya Zanzibar kipo,” alieleza Wasira.

Alisema CCM imeendelea kuzisimamia serikali zake kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa, na kwamba wakati mwingine maendeleo husababisha changamoto mpya.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments