Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, ametoa rai kwa wanasiasa wote nchini kuwa waangalifu na kauli wanazotoa hadharani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Ametahadharisha kuwa baadhi ya matamko ya kisiasa yanaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kijamii na kitaifa iwapo hayatatazamwa kwa makini.
Akizungumza Dar es Salaam kwenye Tamasha la Mtoko wa Pasaka, Dk. Nchimbi amesema wakati mwingine wanasiasa wanateleza katika kauli zao, na hilo linaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wananchi.
“Tunaomba waumini wote wasisite kutukumbusha sisi wanasiasa tunapoteleza, maana kuna wakati mtu anasema neno tu, lakini linaacha madhara kwa taifa. Tunahitaji kuwa na ujasiri wa kusema samahani pale tunapokosea,” amesema.

Katika hotuba hiyo, Dk. Nchimbi pia alihimiza umoja wa kitaifa kwa kuwataka waumini waendelee kuwaombea viongozi wote wa serikali, vyama vya siasa na jamii kwa ujumla, ili taifa liendelee kuwa na mshikamano na amani.
Aliwapongeza taasisi ya Mama Ongea na Mwanao na tamasha la Mtoko wa Pasaka kwa kujitoa kusaidia makundi maalum kama yatima, wagonjwa, wajane na watu walioko katika mazingira magumu, akisema hilo ni jambo linalopaswa kuigwa na kila Mtanzania kama sehemu ya mchango wao kwa taifa.
Dk. Nchimbi amesema kuwa msamaha na upendo ndiyo silaha kubwa ya kujenga taifa lenye mshikamano, hasa katika nyakati za kisiasa ambazo mara nyingi huzua hisia tofauti.
Pia amewaasa waumini na Watanzania kwa ujumla kutafakari upendo na sadaka ya Yesu Kristo kwa binadamu, kwa kujifunza kutoa msamaha wa kweli kwa wengine kama njia ya kujenga taifa lenye maelewano na amani.
Christina Shusho, muandaaji wa mtoko wa Pasaka amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya tamasha hilo wameng’ang’ana na kufika kwenye mafanikio na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zawadi kwa Watanzania waingie bila kiingilio.
0 Comments