Wizara ya Ujenzi, Mahakama mabingwa wapya wa karata Mei Mos

Wizara ya Ujenzi na Mahakama wametwaa ubingwa wa mchezo wa karata kwa wanaume na wanawake katika michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Liti Mkoani Singida.



Katika mchezo wa fainali uliokuwa mkali mchezaji Yusufu Nzomoke wa Wizara ya Ujenzi alimfunga Seif Said wa Wizara ya Uchukuzi kwa magoli 2-1; naye Malkia Nodno wa Idara ya Mahakama alimfunga Farida Chiwanga wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa goli 1-0.

Ushindi wa tatu kwa wanaume umechukuliwa na Magiri Magesa wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP); huku ushindi wa tatu kwa wanawake umekwenda kwa Severina Muyaga wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Bingwa wa wanaume Yusufu amesema ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki mchezo huo,  ulikuwa mgumu katika hatua ya makundi kutokana na kucheza na wachezaji wazoefu wanaoshiriki kwenye michezo ya mashirikisho ya Wizara, Idara, Wakala na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) na Shirikisho la Michezo ya Watumishi wa Umma na Binafsi (SHIMMUTA).  

“Ninamshukuru sana Mungu kwa ushindi huu, pia namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu michezo hii ifanyike, namshukuru Waziri wangu wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega,” amesema Yusufu.

Naye mshindi watatu kwa upande wa wanaume, Bw. Magesa amesema michuano ilikuwa ni mizuri amepambana hadi kufika hatua ya nusu fainali na ameahidi kwenda kujifua zaidi ili mwakani aweze kutwaa ubingwa.

“Mwaka jana katika michezo hii pia nilifika hatua ya nusu fainali, lakini mwaka huu nimeweza kushika nafasi ya tatu, ninaimani nitafanya vizuri zaidi mwakani, nimeisoma nimeisoma michezo yote ya hatua ya makundi na nitakwenda kufanyia kazi,” amesema.

Bingwa wa wanawake, Malkia kutoka Mahakama amesema pamoja na ugeni kwenye michezo hii ameweza kuwafunga wakongwe hadi kutwaa ubingwa wa  mwaka 2025.

Kwa upande wa mshindi wa tatu kwa wanawake Severina amemshukuru mwajiri wake Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuthamini michezo.     

Naye msimamizi wa michezo ya jadi kwa mkoa wa Singida, Eliezer Silvester  wamesimamia vyema na michezo imeenda kama ilivyopangwa.

Hatahivyo, ameiomba serikali kuithamini michezo hii ili iweze kujipambanua zaidi na kuikuza zaidi.
 
Wakati huo huo katika mchezo wa mpira wa kikapu kwa wanaume timu ya Mambo ya Ndani wametwaa ubingwa kwa kuwafunga Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa pointi 133-58. Ushindi wa tatu umekwenda kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) aliyemshinda Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa pointi 92-58.

Katika mchezo wa netiboli timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wameingia fainali baada ya kuwafunga ndugu zao Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa magoli 53-32 mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Mwenge.

Nayo Wizara ya Mambo ya Ndani wameingia fainali sasa kukutana na Ikulu baada ya kuwafunga Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa kwa magoli 58-53.

Nao mabingwa watetezi katika mchezo wa mpira wa miguu TANESCO walimetinga kwa kishindo fainali baada ya kuifunga Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa magoli 4-2.





TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments