Katika mchezo uliopita Tabora United iliifunga Yanga mabao 3-1 Uwanja wa Azam Compex, Chamazi Dar es Salaam, wakati huo ilikuwa chini ya Kocha Mkuu Anicet Kiazmak huku Yanga wakiwa chini ya Miguel Gamondi, ambao wote hawapo na vikosi hivyo kwa sasa.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 58 kwa michezo 22 na Tabora United ina pointi 37, ikishika nafasi ya tano kwa michezo 23.
Akizungumza Tabora jana kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi alisema licha ya kutokuwepo katika benchi kwenye mchezo uliopita Yanga ikifungwa, amepata muda wa kurejea mchezo huo na amebaini namna ataweza kuzuia kutofungwa tena.
Alisema wanauchukulia mchezo huo kwa umakini mkubwa kwa sababu wanahitaji kupata ushindi.
“Tunafahamu mchezo wa kesho (leo) ni mgumu, kwa ujumla mechi zote ni ngumu kwa sababu sisi ni Yanga, hivyo kila timu inapocheza nasi wachezaji wake hujitoa na kuonesha uwezo wao wote,” alisema Hamdi.
Naye Kocha Mkuu wa Tabora United, Genesis Mang’ombe alisema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo na kimejipanga kushinda tena.
“Tulifanikiwa kuwafunga Yanga katika mchezo uliopita ingawa sikuwa sehemu ya benchi la ufundi, na wakati huu mashabiki zetu wanataka tushinde tena, halitakuwa jambo rahisi lakini tumejiandaa hivyo kuanzia safu ya ulinzi hadi washambuliaji, tunategemea ushindi,” alisema Mang’ombe
0 Comments