KIGAMBONI : MSONGAMANO mkubwa wa magari umeshuhudiwa leo Mei 20 katika Barabara ya Kigamboni Kisiwani hadi Kibada, hali inayodaiwa kusababishwa na ufinyu wa barabara hiyo.
Barabara hiyo inayopitia wilayani Kigamboni, ambayo ni moja ya wilaya zinazokua kwa kasi jijini Dar es Salaam, inaruhusu gari moja kupita kwa wakati mmoja kwenda na kurudi upande wa pili. Hali hiyo huzua usumbufu mkubwa hasa nyakati za asubuhi na jioni ambapo magari huwa mengi na madereva hulazimika ‘kutanua’ nje ya njia rasmi, jambo linalosababisha msongamano usioepukika.
Kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi wilayani Kigamboni, idadi ya vyombo vya usafiri imeongezeka maradufu huku miundombinu ya barabara ikionekana kutoendana na kasi ya ukuaji huo.
Kigamboni imeendelea kuvutia wakazi wapya na wawekezaji kutokana na sifa mbalimbali ikiwemo mandhari ya kuvutia ya Bahari ya Hindi, hifadhi ya wanyama ya ‘Dar es Salaam Zoo’, huduma za afya na elimu zinazopatikana kwa urahisi, pamoja na ardhi tambarare inayofaa kwa makazi na biashara.
Hata hivyo, pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kuboresha huduma na miundombinu, changamoto ya miundombinu duni inazidi kujitokeza. Kipindi cha mvua huchangia mafuriko katika maeneo mengi ya wilaya hiyo, huku nyakati za asubuhi na jioni zikitawaliwa na foleni nene za magari.
SOMA: Ulega atoa maagizo ujenzi barabara Kigamboni
Wakazi wa Kigamboni wameitaka serikali kuharakisha upanuzi wa barabara hiyo na kuweka mikakati ya kudumu ya kudhibiti foleni, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mji huo mpya.
0 Comments