Waziri Mchengerwa amshukuru Rais Dkt.Samia kwa kupandisha mishahara, awataka watumishi kuchapa kazi

Siku moja baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara wa watumishi wa Serikali kwa 35% Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemshukuru na kuwaelekeza watumishi chini ya Wizara yake kuwa wazalendo na wabunifu ili kuinua uchumi wa nchi.


Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Mei 2, 2025 wakati alipokuwa akiongea na watumishi wa Mkoa wa Arusha ambapo amesema Wizara yake inasimamia takribani asilimia 76 ya watumishi wote hivyo njia pekee ya kuunga mkono maono ya Mhe. Rais ni kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

" Ndugu zangu ili tuweze kutekeleza maelekezo ya Mhe Rais wetu ni muhimu kutembea katika ndoto zake za kutaka kuwaletea watanzania maendeleo". Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Amesema kufuatia Rais kutoa ongezeko hilo la mshahara wa 35% Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi pekee ambayo imewapatia wananchi wake ongezeko kubwa barani Afrika.

Aidha, amewataka wataalam wa Serikali kwenye Halimashauri zote nchini katika mabaraza ya madiwani kusukuma ajenda za maendeleo na kuonya kwa baadhi ya watumishi wasio waadilifu kubadilika mara moja kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wa Wakurugenzi wa Halimashauri, amewataka kuendelea kusimamia miradi iliyopo kwenye maeneo yao kwa kuzingatia miongozo na sheria huku wakisahihisha makosa yaliyoainishwa ni Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Amewataka waongeze mifumo ya kupata taarifa za ubadhilifu na kuchukua hatua ili kuwadhibiti watumishi hao.

Amewapongeza kwa kazi nzuri ya kuongeza makusanyo na kuendelea kuminya mianya ya upotevu huku akiwataka kubuni vyanzo vipya.

Amewapongeza Wakuu wa Mikoa wote nchini kwa kuimarisha amani na kukuza uchumi kwa kusimamia vema miradi mbalimbali kwenye maeneo yao na kuwasisitiza kuendelea kufanya hivyo na kusisitiza kuwa kamwe siasa isiwe kikwazo cha kufanya maendeleo.

Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda kwa ubunifu wake na kumtaka asiyumbishwe na siasa.




TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments