Akihutubia mamia ya wananchi katika uzinduzi wa kampeni za CCM Jimbo la Ikungi Mashariki, Dkt. Mwigulu alibainisha kuwa ilani ya CCM si karatasi ya maneno pekee, bali ni mwongozo wa vitendo unaoelekeza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa na ya wananchi wa kawaida.
Alisema utekelezaji wa ilani ya CCM umeifanya Tanzania kutazamwa na mataifa mengi barani Afrika kama mfano wa kuigwa kutokana na mafanikio makubwa katika sekta za elimu, afya, miundombinu na uchumi.
“Tunaposema CCM ni chama cha maendeleo hatusemi kwa maneno matupu, tunasema kwa ushahidi wa miradi inayoonekana – barabara, reli, shule, zahanati, hospitali na huduma za kijamii ambazo zinamgusa kila Mtanzania. Huu ndio msingi wa dira yetu ya kitaifa,” alisema.
Dkt. Mwigulu pia alisisitiza kuwa wagombea wa CCM katika ngazi zote ni viongozi wenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi, wakizingatia maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Kura ya CCM ni kura ya maendeleo endelevu, ni kura ya mshikamano na ni kura ya mustakabali bora wa taifa letu,” aliongeza huku akipokea shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria.
Katika mkutano huo, wananchi walionyesha imani kubwa kwa CCM, wakiahidi kuendelea kuunga mkono chama hicho ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi na mipango iliyopo katika ilani ya 2025–2030 inapata nafasi ya kuendelezwa bila kukwama.
Alifu Abdul Singida
0 Comments