Waandishi wa habari wametakiwa kutimiza wajibu wao ipasavyo katika kuhabarisha, kuelimisha na kufichua changamoto zinazohusu jamii, hususan katika nyakati nyeti za uchaguzi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Sosthenes Kibwengo wakati akifungua mafunzo maalum ya waandishi wa habari kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Mkoa wa Singida.
Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa TAKUKURU aliwataka waandishi kuzingatia nafasi waliyo nayo kwa kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya wananchi na viongozi. Alibainisha kuwa vyombo vya habari vina nguvu kubwa ya kuelimisha umma, kufichua vitendo vya rushwa, na kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua.
Aidha, alisisitiza kuwa TAKUKURU ipo tayari kushirikiana na mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusu vitendo vya rushwa, na kwamba ushirikiano huo ni silaha madhubuti ya kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa taifa lenye maadili, haki na maendeleo endelevu.
Akizungumzia kipindi cha uchaguzi, alisema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kuwa walinzi wa maadili ya kitaifa, kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu sera na wagombea, bila upotoshaji au upendeleo. Aliendelea kusisitiza kuwa elimu na uelewa unaotolewa na vyombo vya habari unaweza kuwa msingi wa kuchagua viongozi bora, wenye kuzingatia masilahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
"Waandishi wa habari ni mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii inatambua haki na wajibu wake. Mnapoandika kwa uadilifu na ukweli, mnasaidia taifa letu kupata viongozi bora, kuimarisha demokrasia na kupunguza mianya ya rushwa," alisema.
Mafunzo hayo yalilenga kujenga mshikamano wa pamoja kati ya vyombo vya habari na TAKUKURU, ili kwa ushirikiano huo Tanzania iendelee kuwa mfano wa taifa lenye kupambana kwa dhati na rushwa na kulinda amani yake.
Matukio Mbali mbali ya Picha


Alifu Abdul Singida
0 Comments