Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki, Chief Thomas Mgonto, ameendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwatumikia wananchi kwa vitendo kupitia ziara yake ya "Sikonga na Chief Thomas Mgonto", inayolenga kusikiliza wananchi, kutatua changamoto zao na kuhamasisha maendeleo katika sekta mbalimbali.
Leo, Mbunge Mgonto alitembelea Seminary ya Dungunyi, ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi, walimu na walezi. Katika nasaha zake, aliwahimiza wanafunzi kuwatii walimu wao, kuheshimu wazazi na walezi, pamoja na kuzingatia kwa umakini mafunzo wanayopewa ili kujenga msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
Chief Mgonto alisisitiza kuwa elimu ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla, huku akiwataka wanafunzi kutumia muda wao vizuri darasani na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu ndoto zao.
Ziara ya "Sikonga na Chief Thomas Mgonto" imeendelea kuwa daraja muhimu kati ya viongozi na wananchi, ambapo Mbunge huyo hutembelea shule, vikundi vya kijamii, taasisi na maeneo mbalimbali ya jimbo, akitoa elimu kuhusu maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kushirikiana nao kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.
Wananchi wa Ikungi Mashariki wameendelea kuipokea kwa moyo mkunjufu programu hiyo, wakieleza kuwa imeongeza ukaribu kati ya kiongozi na wananchi, huku ikitoa fursa ya kushughulikia changamoto kwa wakati na kuimarisha maendeleo ya jimbo.

0 Comments