SHILINGI BILIONI 2.4 KUBADILI ULINZI WA WANYAMAPORI KWA TEKNOLOJIA

 Serikali imekabidhi ndege nyuki (drones) 40 kwa Taasisi za Uhifadhi za Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya teknolojia katika kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori nchini.


Ndege hizo zenye thamani ya takriban Shilingi bilioni 2.4 zimenunuliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TWPF), kwa lengo la kuongeza uwezo wa doria za anga, kufuatilia mienendo ya wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati halisi katika maeneo ya uhifadhi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya marubani wa ndege nyuki na kukabidhi vitendea kazi kwa taasisi za uhifadhi na halmashauri jijini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amezitaka taasisi hizo kuhakikisha drones hizo zinasajiliwa na kupata vibali vyote vinavyohitajika kabla ya kuanza kutumika.

Dkt. Kijaji pia ameelekeza taasisi za uhifadhi kuwaandaa wataalam wa ndani kwa ajili ya matengenezo ya drones, hususan matengenezo madogo ambayo yanaweza kufanyika ndani ya uwezo wa taasisi, kutokana na changamoto ya upatikanaji wa wataalam wa matengenezo ya teknolojia hiyo katika maeneo mbalimbali.

Hatua hiyo inalenga kupunguza muda wa kusubiri huduma za matengenezo pindi ndege hizo zinapopata hitilafu na kuhakikisha zinaendelea kutumika kwa ufanisi katika shughuli za ulinzi na uhifadhi.

Mbali na drones, Serikali imekabidhi pikipiki 55 kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Jiji kwa ajili ya kuimarisha shughuli za udhibiti wa migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Kati ya pikipiki hizo, 40 zitatumiwa na Maafisa Wanyamapori wa Wilaya, huku pikipiki 15 zikitolewa kwa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMA) saba, kwa lengo la kuongeza uwezo wa jamii kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uhifadhi.

Kwa mujibu wa Waziri Kijaji, vitendea kazi hivyo vinatarajiwa kuongeza kasi na ufanisi wa operesheni za kudhibiti migongano kati ya binadamu na wanyamapori, hatua itakayosaidia kuokoa maisha ya wananchi, kulinda mali zao na kupunguza gharama za utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi uwandani.

Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Wanyamapori watakaopokea pikipiki hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuzitunza ili ziweze kudumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine, Waziri Kijaji ameitaka TAWA kuimarisha usimamizi wa maeneo ya WMA na kuhakikisha mfumo huo unaleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii kupitia mapato yanayotokana na shughuli za utalii, huku ukisaidia kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mifumo ya kisheria na kiutendaji inayowezesha wananchi kushiriki katika uhifadhi, kwa kutambua kuwa ushiriki wa jamii ni sehemu muhimu ya kuhakikisha rasilimali za wanyamapori zinalindwa na kuleta manufaa kwa wananchi.

Aidha, amewataka Wakuu wa Taasisi za Uhifadhi kusimamia maadili ya watumishi na kuhakikisha vitendo vya ujangili, rushwa na uvunjifu wa sheria havipewi nafasi katika sekta ya uhifadhi.

Amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kulinda heshima ya taaluma ya uhifadhi ili rasilimali za wanyamapori ziendelee kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Katika hafla hiyo, Waziri Kijaji pia ametangaza kufungwa rasmi kwa mafunzo ya matumizi ya ndege nyuki yaliyowashirikisha marubani 52 kutoka TAWA, TANAPA, NCAA na Idara ya Wanyamapori (WD), huku akieleza matumaini kuwa mafunzo hayo yamewaongezea washiriki uwezo wa kiufundi na kitaalamu wa kutumia teknolojia hiyo katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika teknolojia, rasilimali watu na mikakati shirikishi ili kuimarisha uhifadhi endelevu wa wanyamapori na kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Kwa hatua hiyo, matumizi ya drones pamoja na kuongezeka kwa vitendea kazi kwa Maafisa Wanyamapori yanatarajiwa kuongeza uwezo wa Serikali na jamii katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi, hususan migongano kati ya binadamu na wanyamapori, ujangili na ulinzi wa rasilimali za maliasili.





Chanzo Michuzi Blog

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments