TAFITI, USHIRIKIANO VYATAJWA KUWA CHACHU MAENDELEO SEKTA YA MIFUGO.

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewataka wataalamu wa mifugo kutumia matokeo ya tafiti kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji na kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo na mazao yake nchini.

Ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la 49 la Kitaaluma na Mkutano Mkuu wa 50 wa Chama cha Wataalamu wa Mifugo Tanzania (TSAP) Mkoani Iringa, Oktoba 28, 2026,  ameeleza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha Tanzania inafikia utoshelevu wa chakula, hususan protini inayotokana na nyama, maziwa, mayai na samaki kabla ya mwaka 2050.

Aidha, amewataka kutambua kuwa wanaposhughulikia uimarishaji wa minyororo ya thamani, ni muhimu kufikiri zaidi namna ya kuongeza ubora wa bidhaa zinazotokana na mazao ya wanyama na samaki na kuwezesha upatikanaji wa masoko bora, salama, na ya uhakika.

Mwenyekiti wa TSAP, Dkt. Zabron Nziku, ameiomba Serikali kuimarisha ushirikiano na chama hicho ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika kuboresha sera na kutatua changamoto za wafugaji. Amesema chama hicho, kilichoanzishwa mwaka 1973, kina takribani wanachama 1,000 na maandalizi ya kuanzisha jarida lake la kisayansi yamefikia asilimia 85.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amewataka wataalamu kuwasilisha tafiti zenye majibu ya haraka kwa changamoto za wafugaji, amesema licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mifugo mingi barani Afrika, bado kuna changamoto za mifugo kudhoofika na matumizi ya mbinu za jadi za ufugaji.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya mifugo, Dkt. Fabian Madele, amesema Serikali inatambua mchango wa vyama vya kitaaluma na inataka tafiti na ubunifu kuelekezwa katika kutatua changamoto za mifugo na uvuvi kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Mkurugenzi wa kampuni ya ASAS ya usindikaji wa maziwa na mdhamini mkuu wa jukwaa hilo Fuad Abri, amesema tafiti na utaalamu ni muhimu katika kuendeleza sekta ya mifugo na uchumi wa taifa, huku  akiahidi kuendelea kuwaunga mkono wataalamu, akitoa mfano wa biashara ya kuku kutoka Brazil na Congo kwenda Zanzibar, akisema masuala kama hayo yanahitaji majibu ya kitaalamu ili kusaidia wadau kufanya maamuzi sahihi kuhusu uzalishaji na biashara ya mifugo.

Amesema utafiti ni kiungo muhimu kati ya changamoto za wafugaji na suluhisho zake, huku Waziri akiwataka wataalamu kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kuboresha uzalishaji, afya ya mifugo na upatikanaji wa masoko, pamoja na kujiandaa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kongamano hilo limefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Ujasiriamali kwa Minyororo Endelevu ya Thamani ya Mifugo na Samaki.”




TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments