Mbunge wa Bunda Mjini, Mhe. Esther Bulaya, amewataka viongozi na maofisa masuuli katika halmashauri kuacha tabia ya kuwalinda watumishi wanaotuhumiwa kwa wizi na ubadhirifu wa fedha za umma, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinakwamisha uwajibikaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Bulaya amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwatetea watumishi wanaotuhumiwa kuiba fedha za umma, wakiwemo wahasibu wanaodaiwa kuchukua mapato ya vituo vya afya, kwa hoja kwamba mashauri yao yako katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), huku watumishi hao wakiendelea na majukumu yao kama kawaida.
Amesisitiza kuwa uwepo wa mashauri katika TAKUKURU haupaswi kutumiwa kama kisingizio cha kuwakinga watumishi wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu dhidi ya hatua za kinidhamu na kisheria zinazostahili kuchukuliwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Aidha, Bulaya ameeleza kuwa Bunge pamoja na kamati zake hazitavumilia uzembe, ubadhirifu wala vitendo vya wizi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wachache, ambao wanarudisha nyuma juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha fedha zote za umma zilizoibwa au ambazo hazijakusanywa zinarejeshwa haraka serikalini ili ziweze kutumika katika kukamilisha miradi ya maendeleo na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi kote nchini.
Ameonya kuwa ni muhimu kwa kila kiongozi na mtumishi wa umma kutimiza wajibu wake kwa uadilifu, kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha kila fedha inayokusanywa inatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

0 Comments