Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, amesema Serikali haitaruhusu madini yanayozalishwa nchini kusafirishwa nje ya nchi yakiwa ghafi, badala yake itahakikisha yanachakatwa, kusafishwa na kuyeyushwa ndani ya Tanzania ili kuongeza thamani ya rasilimali hizo na kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema msimamo huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na utajiri wake wa madini kwa kujenga uwezo wa ndani wa kuyachakata na kuyaongezea thamani kabla ya kuingia katika masoko ya kimataifa.
Mavunde ameyasema hayo leo, Alhamisi, Novemba 19, 2026, wakati akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TMIC 2026), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji na usafishaji wa madini barani Afrika, huku akieleza kuwa hakuna madini yatakayeruhusiwa kutoka nchini bila kufanyiwa hatua za kuongeza thamani.
"Hakuna jiwe hata moja litatoka kwenda nje ya nchi halijachakatwa, halijasafishwa, halijayeyushwa. Mambo yote yatafanyikia ndani ya nchi," amesema Mavunde.
Akieleza hatua zilizofikiwa katika kutekeleza mkakati huo, amesema Tanzania tayari ina viwanda vinane vya kusafisha dhahabu kwa kiwango cha ubora wa 999.9, huku kiwanda cha GGR kilichopo mkoani Geita kikiwa katika hatua za mwisho za kupata ithibati ya Shirika la LBMA.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kusukuma mbele uwekezaji katika uchakataji wa madini ya nikeli na shaba, ambapo viwanda 16 vinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini. Pia, kuna mradi wa kiwanda kikubwa cha kutenganisha madini tembo (mineral separation plant) katika eneo la Tajiri, wilayani Pangani, mkoani Tanga.
Katika hatua nyingine, Mavunde amebainisha kuwa maandalizi ya mradi mkubwa wa kuyeyusha madini ya ferro-niobium katika Bonde la Songwe, mkoani Mbeya, yanaendelea. Mradi huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa duniani katika uzalishaji wa madini hayo, ukiwa wa nne kwa ukubwa duniani.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini, kuchochea ukuaji wa viwanda, kuvutia wawekezaji zaidi na kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa Watanzania, badala ya nchi kuendelea kutegemea mauzo ya madini ghafi.
Mkutano wa TMIC 2026 umeandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania, ukiwakutanisha zaidi ya wadau 1,700 kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji, changamoto na mwelekeo wa maendeleo ya sekta ya madini nchini.

0 Comments