RAIS SAMIA ATOA MAELEKEZO MAZITO KWA VIONGOZI WAPYA, AHOJI MITAZAMO YA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi mbalimbali aliowaapisha Novemba 2, 2026, kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi zitakazoleta matokeo chanya kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Samia amesema viongozi wanapaswa kuelewa mazingira ya sasa ya dunia, ambako masuala ya haki za binadamu yamekuwa yakitafsiriwa kwa mitazamo tofauti, huku nguvu na ushawishi wa mataifa vikichangia namna yanavyotazamwa na kuhukumiwa.

Amesema katika mazingira ya sasa, nchi zinazotekeleza wajibu wa kulinda haki za binadamu zinaweza kujikuta zikishutumiwa kwa ukiukwaji wa haki hizo, wakati nyingine zinazokiuka haki hizo zikipata mtazamo tofauti kutokana na nguvu na ushawishi wake.

“Katika dunia ya leo mambo yamekuwa juu chini, mwenye haki ataambiwa si mwenye haki na asiye na haki ataambiwa ana haki. Kuna nchi zinafanya vizuri lakini zitaambiwa zinavunja haki za binadamu, na zinazovunja haki za binadamu zinaonekana hazivunji kwa sababu zina nguvu,” amesema Rais Samia.

Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi hao kuwa na utamaduni wa kufuatilia mijadala inayoendelea katika mitandao mbalimbali ya kijamii ili kufahamu taarifa, maoni na tuhuma zinazotolewa kuhusu Serikali, pamoja na mwenendo wa masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesisitiza kuwa viongozi hawapaswi kupuuza mijadala inayohusu taasisi na maeneo yao ya kazi, bali wanapaswa kuhakikisha wanatoa ufafanuzi na majibu stahiki kwa hoja zinazowasilishwa, ili wananchi wapate taarifa sahihi na kuepusha upotoshaji.

Rais Samia ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikikabiliwa kwa muda mrefu na tuhuma zinazohusiana na masuala ya haki za binadamu, akibainisha kuwa suala hilo ni sehemu muhimu ya utawala bora linalohitaji viongozi kuwa makini, wawajibikaji na wenye uwezo wa kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali.

Amesisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kuchukulia nafasi walizopewa kama dhamana ya kuwatumikia wananchi, kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kulinda taswira ya taasisi wanazoziongoza kupitia utendaji wenye matokeo yanayoonekana.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments