SERIKALI YAONGEZA NGUVU KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA WALIMU

 Serikali imesema itaendelea kuajiri walimu kila mwaka na kujaza nafasi zinazojitokeza kutokana na walimu wanaokoma utumishi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Vijijini, Dkt. Jasson Samson Rweikiza, aliyetaka kufahamu ni lini tatizo la upungufu wa walimu katika shule nchini litakoma.

Dkt. Dugange amesema Serikali inatambua changamoto ya upungufu wa walimu inayochangiwa na ongezeko la udahili wa wanafunzi kutokana na utekelezaji wa sera ya elimu bila ada, sambamba na kuongezeka kwa idadi ya shule mpya zinazojengwa nchini.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikiendelea kuajiri walimu kila mwaka kulingana na mahitaji yaliyopo. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2025/26, jumla ya walimu 64,772 wameajiriwa nchini.

Kati ya hao, walimu 15,054 wameajiriwa katika mwaka wa fedha 2025/26 na kupangiwa katika vituo vya kazi, hususan maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi ya walimu.

Aidha, amesema Serikali inatarajia kuajiri walimu zaidi katika mwaka wa fedha 2026/27, ambao watapangiwa katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa walimu.

Mbali na kuendelea na ajira mpya, Serikali pia itaendelea kujaza nafasi za walimu wanaokoma utumishi kutokana na sababu mbalimbali, pamoja na kutumia walimu wa kujitolea kwa kuzingatia Mwongozo wa Kujitolea katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2026.

Hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza upungufu wa walimu na kuhakikisha wanafunzi katika shule za msingi na sekondari wanapata huduma bora za elimu nchini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments