Recent-Post

Kaya 644 kurejea Magomeni kota baada ya miaka minne TUESDAY FEBRUARY 16 2021


 Dar es Salaam. Kaya  644 zilizohamishwa kwa muda ili kupisha ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni kota zinatarajiwa  kurejea eneo hilo Aprili, 2021 baada ya ujenzi kukamilika.

Hadi leo Jumanne Februari 16, 2021 ujenzi huo  unaotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ulioanza Oktoba 2016 umekamilika kwa asilimia 91.

Rais John Magufuli aliagiza ujenzi huo akitaka ukamilike ndani ya mwaka mmoja lakini ulikuwa ukisimama kwa vipindi tofauti kwa kile kinachoelezwa kuwa ni changamoto ya fedha.

Akizungumza leo mara baada ya kutembelea mradi huo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya amesema ameridhishwa na mradi huo kwa kuwa unaenda vizuri na kwa ubora uliokuwa unatarajiwa.

 Kasekenye amesema Aprili, 2021  ujenzi huo utakuwa umekamilika na kuanza taratibu za wananchi waliokuwa wanaishi awali kuhamia na kuanza kuishi kwenye majengo hayo mapya.

“Baada ya kukagua na kujiridhisha kuwa ujenzi uko asilimia 91,nimewaeleza TBA watakapomaliza mradi huu waangalie na maeneo mengine watakayoweza kutekeleza mradi kama huu,” amesema

Mtendaji Mkuu wa TBA,  Daudi Kondoro amesema, “kama mlivyoona mandhari ya ndani na nje, tupo kwenye hatua za mwisho, fedha tumepata na vifaa vipo na kama tulivyoeleza utekelezaji unafanyika usiku na mchana ifikapo Aprili tutakuwa tumekamilisha.”

Post a Comment

0 Comments