LUNYAMILA: KWA HILI LA NAMUNGO, TFF WANASTAHILI PONGEZI

 

Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na ile ya kombe la Shirikisho Afrika imezidi kushika kasi katika viwanja mbalimbali barani humu, ambapo kwa Ligi ya Mabingwa michuano hiyo ipo katika hatua ya makundi huku ile ya Shirikisho ikiwa katika hatua ya mtoano.

Hongera kwa Simba ambao wameanza vyema kibarua chao kwa ushindi wa ugenini dhidi ya AS Vita katika mchezo wao wa kwanza wa kundi A, ushindi huo unatoa mwanga mzuri kwa Simba katika kuhakikisha wanafikia malengo yao ya angalau kufika nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Simba wanastahili pongezi kutokana na uimara mkubwa waliouonyesha kwenye mchezo huo kwa kulinganisha na mchezo wa mwisho dhidi ya AS Vita, katika hatua kama hiyo msimu wa 2018/19 ambapo katika msimu huo Simba walikubali kipigo cha mabao 5-0.

Jukumu lililosalia kwa Simba hivi sasa ni kuhakikisha moto walioanza nao hauzimiki, bali wanaendelea kushikilia hapo hapo na ikiwezekana kuongeza ufanisi zaidi katika michezo yao mitano iliyosaliwa nayo, ili kufuzu hatua ya robo fainali na ikiwezekana nusu fainali kama yalivyo malengo yao.

Kama Watanzania wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha tunaendelea kuwaombea kheri Simba kwani mafanikio yao ni mafanikio ya soka la Tanzania kwa ujumla, kama tujuavyo kama Simba watafika mbali kwenye michuano hii basi Tanzania itazidi kuvuna pointi nyingi kiasi cha kuongeza namba za timu shiriki kutoka mbili za sasa hadi nne.

Lakini pia pongezi kwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika Namungo, ambao wao wamefanikiwa kupenya hadi katika hatua ya mtoano ya michuano hiyo na kwa sasa wanaikimbizia tiketi ya hatua ya makundi.

Namungo inayoonekana kupitia kwenye kigumu ndani ya Ligi Kuu Bara, imeonyesha uhai mkubwa katika michuano ya kimataifa kwa kuziondosha timu mbili kutoka nchi za Sudani na Sudani ya kusini.

Licha ya mafanikio ya michuano hiyo ya kimataifa, lakini kuna mdudu ameingia ambaye anafanya kuanze kuwepo mashaka juu ya ufanisi na mafanikio ya michuano hiyo, changamoto hiyo ni ile ya baadhi ya klabu kuanza kutumia faida ya kuwepo maambukizi ya Corona kwenye baadhi ya nchi kama sehemu ya kidhoofisha wapinzani.

Ishu hii ilianza kuibuka wakati wa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani CHAN iliyofanyika nchini Cameroon kuanzia Januari 16 hadi Februari 7, mwaka huu.

Kupitia michuano hiyo kocha wa DR Congo, Florent Ibenge aliweka wazi kwamba baadhi ya nyota wa kikosi chake pamoja na yeye mwenyewe walipakaziwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona ili kuidhoofisha timu yao.

Baada ya kuwa kama stori kwa wenzetu tukio hilo pia limetokea kwetu Watanzania kupitia klabu ya Namungo ambayo ilipata wakati mgumu nchini Angola kufuatia kudaiwa baadhi ya nyota wake wameambukizwa virusi vya Corona.

Hali hiyo ilileta sintofahamu kubwa kiasi cha Shirikisho la soka Tanzania (TFF), kuingilia kati na kuwasiliana na Shirikisho la soka Afrika (CAF), na kupelekea mchezo huo kufutwa kupisha uchunguzi.

Kwa hili nadhani TFF wanastahili pongezi kubwa kwa kusimamia maslahi ya Taifa katika mchezo wa soka.

Uchambuzi wa Lunyamila kupitia gazeti la Championi Jumatatu

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments