Dar es Salaam. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapunguzia watoto majukumu ya nyumbani ili kuwawezesha kupata muda wa kujisomea na kupumzika.
Majaliwa amesema hayo leo Jumanne Februari 23, 2021 wakati akizungumza na walimu, wanafunzi na wazazi baada ya kukagua miundombinu ya shule ya msingi Mitope, Ruangwa mkoani Lindi.
Amesema iwapo watoto watapata muda mzuri wa kujisomea na kupumzika itawasaidia kuwaongezea ufaulu kwenye masomo yao na kutimiza ndoto zao.
Mbali na hilo, Majaliwa amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wananunuliwa vifaa vyote vinavyohitajika shuleni zikiwemo sare, madaftari sanjari na kufuatilia mienendo yao kielimu.
”Wazazi tufuatilie na kujiridhisha kama watoto wetu wanafika shule na kuingia madarasani. Pia tuwe tunakagua madaftari yao na pale tunapoona hawafanyi vizuri tuwasiliane na walimu,” amesema Majaliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa amesema atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake kuendelea kusimamia vizuri shughuli za maendeleo.
0 Comments