Recent-Post

Profesa J aeleza haya baada ya kutajwa na Magufuli


Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu Profesa J amesema Rais wa Tanzania, John Magufuli kuomba apigiwe wimbo wa Baba ni mwendelezo wa kiongozi mkuu huyo wa nchi kuwa shabiki wake namba moja.

Leo Alhamisi Februari 25, 2021 katika uzinduzi wa studio za Channet Ten na Magic FM jijini Dar es Salaam, kiongozi huyo aliomba kupigiwa wimbo wa Baba  wa msanii Stamina aliyemshirikisha Profesa J na kubainisha kuwa una ujumbe mzuri.

Wimbo huo unamzungumzia kijana anayehangaika kutafuta maisha na kumsema baba yake kwamba hali aliyonayo inatokana na mzazi wake huyo kushindwa kutafuta fedha wakati wa ujana wake, mzazi huyo kumjibu jinsi alivyohangaika kumlea licha kuwa si mwanaye wa kumzaa lakini alihakikisha anapata mahitaji yote.

Akizungumza na Mwananchi Digital Profesa J ameeleza kuwa Rais Magufuli alishawahi kusema ni shabiki wa muziki wake, hivyo kitendo cha kuomba wimbo wa Baba ni kuonyesha bado ni shabiki wa muziki wake na ni jambo kubwa kwake.

“Alipokuja Kilosa alisema yeye ni shabiki wa muziki wangu, hivyo kitendo cha leo kuutaja wimbo wa Baba ni kuonyesha kuwa ameendelea kuwa shabiki wangu na ni shabiki wa muziki mzuri hii kwangu ni jambo kubwa.”

“Kitendo cha mkuu wa nchi kutamka hadharani kuwa wimbo wa Baba una maudhui mazuri hii inaleta nguvu ya kuendelea kufanya kazi bora nzuri kwa manufaa ya kizazi kijacho,” amesema.

Post a Comment

0 Comments