Stamico yakamilisha ujenzi wa kiwanda cha kusafisha madini nchini

 Stamico pic

Waziri wa Madini, Dotto Biteko akikagua kiwanda chenye mtambo wa kusafisha madini uliojengwa wilayani Ilemela mkoani Mwanza kwa Sh8.9 bilioni. Picha na Mgongo Kaitira.

Mwanza. Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kwa kushirikiana na Kampuni ya Lozera ya nchini Dubai imekamilisha ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kusafisha madini cha Mwanza Precious Metal Refinery (MMPR) kilichoko wilayani Ilemela mkoani hapa.

Ujenzi huo ulianza Machi 15, 2020 ambapo zoezi la ufungaji wa mtambo wa kusafisha madini hayo limekamilika huku mtambo ukitarajiwa kuanza kusafisha dhahabu mwezi Machi  1, 2021.

Akizungumza leo Jumatatu, Februari 15,  2021 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, Dk Venance Mwasse amesema mtambo huo umegharimu Sh8.9 bilioni na utakuwa na uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku.
Kukamilika kwa mtambo huu kutawezesha kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku ila unaweza kupanuliwa na kuweza kusafisha hadi kilo 960 za dhahabu kwa siku," amesema Dk Mwasse.
Ameongeza kwamba lengo la mtambo huo ni kuongeza thamani ya madini ya dhahabu yanayochimbwa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Tumezoea kuona madini yanasafishwa nje ya nchi na kusababisha Serikali kupoteza mapato yake lakini kupitia mradi huu tutaongeza mapato kwa nchi kupitia mrabaha na kodi mbalimbali," amesema.
Akizungumza baada ya kutembelea mtambo huo Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema pamoja na kuchangia kwenye pato la Taifa mradi huo utazalisha ajira za ndani na nje kwa Watanzania.
Nimeambiwa mradi huu unategemea kutoa ajira za ndani 120 na hii itasaidia kuongeza mnyororo wa fedha kwa Watanzania," amesema Biteko.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments