Recent-Post

WATUMISHI 15 GEITA WASIMAMISHWA KAZI

Chato. Baraza la madiwani  halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita limewasimamisha kazi watumishi 15 wa idara mbalimbali kutokana na ubadhilifu wa Sh3.9 bilioni za miradi ya maendeleo.

Miongoni mwa watumishi hao sita ni  wa idara ya manunuzi ,wengine sita ni watendaji wa vijiji,  wauguzi wawili na ofisa kilimo wa kata ya Inchwankima aliyeondoka kwenye kituo cha kazi kwa miezi mitatu bila taarifa huku akiwa ametoroka na Sh300,000 za wananchi.

Uamuzi huo umetangazwa leo Alhamisi Februari 18, 2021  mwenyekiti wa baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, Batholomeo Manunga aliyebainisha kuwa wamemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuunda tume ya uchunguzi itakayohusisha baadhi ya madiwani na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.

Ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kuichunguza miradi yote iliyotengewa fedha lakini haijatekelezwa, kumtaka mkurugenzi kuwachukulia hatua zaidi watendaji wa vijiji ambao hawajasoma taarifa za mapato na matumizi tangu mwaka 2018.

Baraza hilo lililofanyika jana Jumatano Februari 17, 2021  lilianza na vuta nikuvute baada ya madiwani kugoma kuendelea na kikao kutokana na  taarifa za miradi inayotekelezwa kutowekwa.

Mkuu wa Wilaya ya Chato,  Charles Kabeho amesema hatamvumilia mtumishi yeyote anayerudisha nyuma maendeleo ya wilaya hiyo na kusema tayari ameanza kwa kuwakamata baadhi ya watumishi na kuwafikisha kwenye vyombo vya uchunguzi kwa hatua zaidi .

Post a Comment

0 Comments