Wilaya Ya Ulanga Na TADB Kuwekeza Kilimo Cha Karanga Mti

 Mkuu wa wilaya ya Ulanga Mhe. Ngollo Malenya amepokea ujumbe kutoka  Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania TADB uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji ndugu Japhet Justine katika kuangazia namna Wilaya ya Ulanga inaweza kuwekeza na kunufaika na  kilimo cha Karanga mti (Macademia).


Wilaya ya Ulanga ni wilaya ambayo ina ardhi yenye rutuba na hali ya hewa inayowezesha zao la karanga mti kustawi vizuri. Serikali ya wilaya hiyo imekwishatenga ekari 9025 kwaajili ya kilomo cha Karanga Mti (Macademia)

"Kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameweka kilimo kuwa kipaumbele katika awamu hii ya tano na kusisitiza kila wilaya kuwa na zao linaloitambulisha sisi wana Ulanga tumeona vyema kufungua fursa ya uwekezaji kwa kilimo cha karanga miti. Tunataka Wilaya yetu itambulike kwa kilimo hiki." Alisema Mkuu wa Wilaya katika mkutano mfupi na ujumbe wa TADB pamoja na viongozi wa halmashauri ya Ulanga.

Mradi huu wa Karanga mti unatarajiwa kuwa moja ya miradi mikubwa na wakipekee kwa afrika Mashariki na kati

Akitoa ripoti ya namna ambavyo wananchi Wilayani hapo wanavyoshiriki katika mchakato wa kuanza kilimo cha Karanga miti, Afisa Ushirika wa halmashauri Bwana Charles Eman alibainisha kuwajengea wananchi uelewa wa ushirika na manufaa ya kuwa kwenye ushirika. "Kupitia ushirika wananchi wameweza kujiunga katika vikundi na wako tayari kushiriki kikamilifu." Alisema

Cosmas Misinzo mpima  ardhi wa halmashauri nae alieleza namna ambavyo wamejipanga katika kufikia malengo haya. "Kwa sasa tumetenga zaidi ekari elfu tisa. Kati ya hizo ekari 8900, zitatumika kama mashamba. Tumepima maeneo haya yote na jumla ya vitalu 107 vimepatikana. Vitalu hivi ni vyenye wastani wa ukubwa wa ekari 60. Pamoja na kuwa tulikuwa na ufinyu wa rasilimali, tulijituma kwa bidii kuhakikisha wilaya yetu inaweza kunufaika na wanachi wetu wakiwa na uhakika wa kipato." Alisema.

Akizungumzia uwepo wa TADB katika wilaya hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Japhet Justine alisema " TADB ni jukumu lake kuchagiza kilimo nchini. Hapa Ulanga tuko tayari kuwekeza kwa wakulima wetu. TADB itatoa mkopo uliohimilivu. Wakulima wetu wataanza kurejesha baada ya kuanza kuvuna karanga miti. Tunaelewa kuwa hili ni zao ambalo linatoa matunda baada ya miaka minne."

Kwa kutambua hili TADB inadhamiria kuwawezesha wakulima Ulanga sio tu kwa mtaji bali pia kwa kuweka afisa kilimo atakayesimamia na kuwashauri wakulima kwa kilimo chenye tija.

Pamoja na kushiriki kikao hicho Mkuu wa Wilaya na ujumbe kutoka TADB walitembelea shamba la karanga miti linalomilikiwa na kampuni ya Tanzania Nuts Limited. Katika shamba hilo Mkuuwa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB waliwezakuona uzalishaji wa miche ya Karanga Miti na shamba la karanga miti. Katika shamba hilo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB waliweza kujifunza namna miche ya karanga miti inavyoandaliwa hadi wakati wakupanda.

"Hili ni zao la jamii ya karanga ambalo thamani yake inashindana na ile ya zao la korosho. Hii ni fursa kwa vijana kuwekeza katika kilimo hiki. Nimefurahi kuona vijana kutoka chuo cha SUA wakiwa hapa na wanafurahia kazi yao. Hii inahamasisha vijana kufahamu kuwa kilimo kinahitaji uvumilivu ilikuweza kufanikiwa. Ni wakati sasa vijana kubadili fikra na kuelewa kuwa fursa zipo shambani." Alisema ndugu Japhet

 Akizungumzia ujio wa TADB Wilayani Ulanga, Mhe. Mkuu wa Wilaya alisema " tumejipanga na tuko tayari kuweza kuifungua wilaya yetu. Tunataka tufahamike duniani kwa kuzalisha karanga miti."

Kaimu Mkurugenzi wa halmshauri ndugu Andreas Whero alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa jitihada zake binafsi kwa za kuhamasisha halmashauri kuona fursa hii adimu ya kilimo cha karanga miti. "Tunakushukuru sana Mhe. Mkuu wa Wilaya. Tulikua tumezoea kudhani kuwa kilimo ni mpunga na mahindi tu. Sasa tumefahamu kuhusu karanga miti na tuko tayari kuanza." Alisema.

Kilo moja ya Karanga miti huuzwa kwa zaidi ya shilingi elfu kumi na tano. Karanga miti inatajwa kuwa na fauda mbalimbali na virutubisho vingi muhimu kwa mwanadamu.
 

Post a Comment

0 Comments