YANGA WAPUMZISHENI TFF, BODI YA LIGI, ANZENI NA TIMU YENU

 


Tumekubaliana mara zote kwamba tuseme ukweli kila inapohitajika kufanya hivyo kwa ajili ya maendeleo ya mpira wetu, ni jambo zuri.


Hata hivyo, hii haitupi nafasi ya kusemasema ili mradi, kulalamika bila ya sababu ya msingi au kushutumu na kushambulia taasisi fulani au watu bila ya kutulia na kuwazua mambo kwanza.

Hapa nawazungumzia wale baadhi ya mashabiki wa Yanga waliofanya vurugu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji Mbeya City.

Ukiangalia mwamuzi, hakika alijitahidi sana, aliifanya kazi yake vizuri hata kama ni makosa yalikuwa madogo sana ya kibinadamu. Angalia bao la Yanga, kwa mwamuzi asiye makini ni vigumu sana kuona halikuwa bao au la. Lakini unaona mwamuzi huyo kaifanya kazi yake vizuri, utata unabaki kwetu lakini uhalisia, lile ni bao.


Rudi kwenye tukio lililosababisha penalti, hakuna ubishi beki wa kushoto wa Yanga, Yassin Mustapha yuko ndani ya eneo la 18 na ameshika ule mpira, haina mjadala na mwamuzi kaifanya kazi yake kwa kufuata sheria 17 za soka.


Hapa ndipo unapaswa kuanza kujiuliza, wale wanaolalamika kipi hasa wanachokilalamikia na ukiwakuta wengi wao wanazungumzia kwamba Deus Kaseke aliangushwa na beki wa Mbeya City wakati wakikimbia, inawezekana waligongana na mwamuzi msaidizi hakuonyesha kweli kama kuna faulo.


Mwamuzi huyo msaidizi ndiye alionyesha kuwa mpira umefunga msitari na Yanga ikaandika bao, sasa vipi ionekane kawaonea pale? Kuna mengi sana ya kujiuliza.


Ajabu zaidi wakati haya yanatokea ambayo inaonyesha wazi kuwa mechi hiyo haikuwa na makosa ya mwamuzi kufanya watu wapandwe jazba hivyo. Maana kama ni jazba, hata Mbeya City nao wangeweza kufanya hivyo kwa kisingizio cha mpira haukuwa umevuka msitari.

Lawama zinaelekezwa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tena wengine wakiwadhihaki viongozi wao kwa sababu zisizokuwa na msingi, si sahihi.


Hakuna sababu hata kidogo ya kusema maneno ya kashfa kwa viongozi wa taasisi hizo kwa kuwa si kweli wao kuwa pale ndio imepitishwa watukanwe au dhihaka ya kila aina.


Si saw ahata kidogo watu kuamini kila upungufu sababu kuu itakuwa ni imetokana na TFF au TPLB. Jiulize, vipi mashabiki hao hawazungumzii kuhusiana na kiwango cha kikosi chao na kuangalia wachezaji wao walifanya kipi kilichokuwa sahihi kuipigania timu yao? Kiwango walichokionyesha dhidi ya Mbeya City ni sahihi kweli, ni kile ambacho kinaweza kuonyesha Yanga ilionewa?


Yanga ilipiga mashuti mangapi yaliyolenga lango ndani ya dakika 90? Sote tunajua hata matano hayafiki na mengi si mashuti sumbufu! Nafasi walizotengeneza ni ngapi na walizitumiaje? Tunajua kuhusiana na ukweli lakini baadhi wanajaribu kutaka kuonyesha wameumizwa na hili nimelisema mara nyingi sana, zile tabia za kutaka kuwaonyesha wengine kwamba wewe ni shabiki kindakindaki na umeumia sana. Soka ni starehe yako, furahia na umia kivyako si lazima uweke matangazo, haina msaada wowote.

Kikosi cha Yanga hakikuonyesha soka safi, soka la kuitisha Mbeya City na kuiweka katika wakati mgumu kiasi cha kusema walilazimika kubebwa na mwamuzi. 

Inapendeza sana kama mashabiki wakawa wanatafakari vitu kabla ya kuanza kuvifanyia kazi, pia wajiondoe katika ile hali ya kutaka kila jambo lazima kuwe na vurugu au matusi.

Watu wasiojielewa pekee ndio wanaweza kujivunia uwezo wa wa kutukana au kufanya vurugu. Anzeni kumhoji Kocha Kaze kutokana na aina ya uchezaji, kikosi chake kwa maana ya ushambulizi, idadi ya mabao ya kufunga na kadhalika. Wapeni maswali wachezaji wenu, waambieni waongeze juhudi waipambanie timu, wanachofanya sasa, bado!

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments