DC Shimo ataka wanaofuga fisi majumbani kuwaondoa

Nyang’hwale. Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale,  Wilson Shimo  amewataka wananchi  wanaofuga fisi  majumbani mwao kuwaondoa kwa kuwa ni kosa kisheria.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 10, 2021 baada ya kushika kasi kwa matukio ya watu kushambuliwa na wanyamapori hao.

Wataalamu wa jadi waliwasaka na kuwaua fisi 24 wilayani Nyang’wale Mkoa wa Geita baada ya wanyama hao kuua na kujeruhi watu, na sasa uongozi wa wilaya hiyo utaanza msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini watu wanaowafuga.

Uamuzi huo umetokana na madai ya fisi wengine kufugwa kwa lengo la kutafuta kitoweo huku wengine wakiwatumia kama chombo cha usafiri.


Kwa kipindi cha mwezi mmoja fisi wamewaua watu watatu na kujeruhi wengine watano pamoja na kuua mbuzi.

Katika maelezo yake, Shimo amesema amepokea taarifa za baadhi ya wakazi kufuga fisi majumbani na wanyama hao wameanza kuzurura mitaani kusaka chakula.

“Uzoefu unaonyesha watu wanaofuga mnyama huyo humtumia kama chombo cha usafiri huku wengine wakimtumia kutafuta chakula kwa ajili ya familia niwatake wawachie warudi msituni kabla msako haujaanza kuwafuga nyumbani bila kibali ni kosa kisheria.”

“Fisi anafugwa maalum kwa ajili ya kuwinda kitoweo ndio maana aina hii ya fisi wamefundishwa wakimkamata mbuzi hamli bali atambeba hadi nyumbani kwa anayemfuga na anapeleka kitoweo na kisha atarudi tena kukamata mwingine,” amesema Shimo.

Mkuu huyo wa wilaya  amewataka  wazazi kuwalinda watoto wao na kutowaruhusu kutembea wenyewe.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments