Halmashauri ya Songea yaingia mkataba kukusanya mazao

 Na. Albano Midelo, Ruvuma

Halmashauri ya wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imeingia mkataba na kampuni ya West Food Comp LTD ya kutoka Makambako Mkoani Njombe kwa ajili ya kukusanya ushuru wa mazao.


Makubaliano ya mkataba huo yamefanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa kuwekeana saini baina ya Mkurugenzi wa Kampuni na Uongozi wa Halmashauri.

Akisaini mkataba huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  Tanu Kameka ametoa wito kwa Kampuni hiyo kufanya kazi waliyoomba kwa ufanisi kwasababu Serikali inategemea mapato kwa ajili ya kutekeleza majukumu  yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni hiyo Godwin Chengula, ameahidi kufanyakazi kwa ufanisi  na kwamba ana uzoefu katika kazi ya ukusanyaji ushuru ambayo ameifanya katika maeneo ya Wilaya za Ulanga ,Ifakara ,Makambako na Manispaa ya Songea

Naye Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Rajabu Lingoni amesema katika kuboresha ukusanyaji wa mapato vikao vya kisheria vilikubaliana kumpata mzabuni atakayefanya kazi ya ukusanyaji wa ushuru wa mazao badala ya kuendelea kuwatumia mawakala.

“Maamuzi hayo yamefikia baada ya kubaini udanganyifu mkubwa katika ukusanyaji wa ushuru,unaofanywa na baadhi watendaji wa Kata kupitia mawakala wao kitendo ambacho kilikuwa kinakwamisha jitihada za Halmashauri katika kutekeleza majukumu yake’’,alisisitiza.

Lingoni amesema jumla ya vizuio 15 vimeanishwa na vimekabidhiwa kwa mzabuni ambavyo vitatumika katika kukusanya ushuru wa mazao katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2022.

Hata hivyo amesema mzabuni anatakiwa kukusanya ushuru kwa kuzingatia taratibu,kanuni na sheria za ukusanyaji wa mapato zilizowekwa na Serikali.

Kwa upande wake Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri hiyo Noel Chengula ameutaja utaratibu wa kutoa zabuni katika kazi ya ukusanyaji ushuru ni kitendo kitakachoongeza ufanisi na kuondoa usumbufu na gharama za kuwalipa mawakala ambao awali walikabidhiwa jukumu hilo.

Chengula amesema jambo hilo litapunguza changamoto ya madeni kwa baadhi ya Watendaji wa Kata, Vijiji na mawakala na kwamba gharama za ufuatiliaji,na fedha za makusanyo zitafikishwa benki kwa wakati.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments