RAIS SAMIA AFANYA MABADILIKO KATIKA BARAZA LA MAWAZIRI...AONYA DHARAU KAZINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. 

Na Damian Masyenene
KUFUATIA Uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Isdor Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na kumteua Katibu Mkuu Kiongozi mpya.

Rais Samia ametangaza mabadiliko hayo leo saa 9 Alasiri katika hafla ndogo ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

Katika uteuzi huo, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi wa Tanzania nchini Japan, Hussein Yahya Katanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi akichukua nafasi ya Dk. Bashiru Ally ambaye ameteuliwa kuwa Mbunge.

Kwa upande wa mabadiliko ya baraza la mawaziri, Rais Samia Suluhu Hassan amemhamisha aliyekuwa Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu kwenda Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Seleman Jaffo akipelekwa kushika nafasi ya Ummy Mwalimu.

Mwigulu Nchemba amepelekwa wizara ya Fedha na Mipango akisaidiwa na Hamad Masauni na nafasi yake katika Wizara ya Katiba na Sheria kuchukuliwa na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Paramagamba Kabudi akisaidiwa na Jofrey Mizengo Pinda.

Balozi Liberata Mulamula ameteuliwa kuwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku naibu wake akiteuliwa Mbarouk Nassoro Mbarouk.

Kwa upande wa Wizara ya Nchi ofisi ya Rais, utumishi na Utawala bora, ameteuliwa Mohamed Omary Mchengelwa, huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Capt. George Mkuchika akipangiwa kazi nyingine.

Wizara ya Uwekezaji imerejeshwa katika ofisi ya Waziri Mkuu na kutolewa ofisi ya Rais, huku Geoffrey Mwambe akiteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo na Prof. Kitila Mkumbo akipelekwa wizara ya Viwanda na Biashara.

Pauline Gekul ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa wizara ya Michezo, Sanaa, Utamaduni na Michezo, huku aliyekuwa naibu waziri wa wizara hiyo, Abdallah Ulega akipelekwa wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa naibu waziri.

Naye, Mwanaidi Ally Hamis ameteuliwa kuwa naibu waziri wa pili katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. 

Akitangaza mabadiliko hayo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuondoka kwa Dk. Philip Mpango katika Wizara ya Fedha na Mipango kumempa nafasi ya kulitazama baraza lote la mawaziri na kufanya mabadiliko kidogo.

"Nimeona niwabadilishe kwa sababu tangu mumeapa ni muda mfupi kuona nani ameshindwa, tunaanza na hawa awamu ya sita, jinsi tunavyokwenda tutaona nani tunakwenda nae na nani tunamuacha.

"Naibu mawaziri mkatumike vizuri, kuna kudharauliana, naibu anadharau waziri na waziri nae anadharau naibu, kazi ni kazi sitaki kusikia kingine," amesisitiza.

Katika upande mwingine, Rais Samia amefanya uteuzi wa wabunge watatu ambao ni Dk. Bashiru Ally, Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya bandola tz HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments