WACHEZAJI KUGEUKA MABONDIA HII NI MBAYA KWA AFYA YA SOKA LETU

 


 
LIGI Kuu Tanzania Bara inazidi kukata mbunga hasa kwa mzunguko wa pili ambapo kumekuwa na matukio mengi  mazuri na mabaya ndani ya uwanja.

 Ukiweka kando malalamiko kuhusu waamuzi pia wachezaji nao kwa sasa naona wamebadilika. 

Wachezaji wengi wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kusaka ushindi ndani ya uwanja. Wanaoenkana kuegeuza uwanja kuwa ulingo kama ambavyo mabondia wanafanya.

 Jambo hilo limekuwa likifanya wengine waumie huku wengine wakicheza kwa hofu. Katika hili lazima wachezaji wabadilike na kucheza mpira kwa amani. 

Waachane na tabia ya kugeuka kuwa mabondia kwa kupigana ama kuchezeana vibaya ndani ya uwanja.

Maamuzi yao ndani ya uwanja yamekuwa yakiwagharimu wachezaji wenzao hasa pale wanapoumia katika harakati za kusaka ushindi.

Katika hili ni muhimu kwa kila mchezaji kuwa mlinzi wa mchezaji mwenzake kwa kuwa hali haijawa salama kwa nyakati hizi ukianza mzunguko wa kwanza na huu wa pili.

 

Jambo moja la msingi la kufanya kwa wachezaji ni kujali mpinzani wake na kuamini kwamba mpira sio vita bali ni burudani.

 

Ile burudani inapopotea na kuanza kuwa ni vita ndani ya uwanja hapo tunashuhudia balaa kubwa. Imekuwa kawaida kwa sasa ndani ya uwanja kushuhudia buti za maana pamoja na viwiko kwa wachezaji.

 

Hali hii ni mbaya hasa kwa afya za wachezaji wetu ambao kazi yao ni mpira. Kati ya vitu ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya mchezaji ni maumivu anayopata akiwa kazini kwa kuumizwa.

 

Wapo ambao mpaka leo hawakukubali kurudi uwanjani kwa kuhofia kuumizwa pia wapo ambao mpaka muda huu wanatibu majeraha ambayo waliyapata.

 

Ipo wazi kwamba mchezo wa mpira ni mchezo wa kutumia nguvu ila ifike mahali kwamba nguvu itumike pale inapostahili.

 

Wapo wale ambao wanachukua sheria mkononi na kutumia ubabe hili halipo sawa ni muhimu wachezaji kubadilika na kucheza kwa ustaarabu ndani ya uwanja.

 

Kwa sasa kumekuwa na maumivu mengi kwenye soka hasa kutokana na kuripotiwa baadhi ya matukio ambayo hayaleti picha nzuri. Muhimu kwa wachezaji kuwa makini ndani ya uwanja muda wote

 

Endapo inaweza kutokea tukio baya ambalo labda mwamuzi hajaona ama wachezaji hawajaona itakuwa ni hatari kwa timu nzima pamoja na mchezaji mwenyewe.

 


Hivyo jambo la msingi wachezaji wote wanapaswa wajue kwamba mlinzi wa mchezaji mwingine ni mchezaji mwenyewe uwanjani.

 

Kama linatokea tatizo anapaswa atoe huduma kwanza kabla ya kuangalia matokeo ambayo anayapa kipaumbele kwani uhai wa mchezaji ni bora muda wote kuliko matokeo yenyewe.

 

Itakuwa ni wakati mzuri pia kwa timu zote kujifunza kuwa na 'Fair Play' uwanjani ili kutoa mwanya kwa wachezaji kuwa na maamuzi sahihi kuhusu afya za wachezaji.

 

Ikitokea hivyo itawajengea uwezo wachezaji kujali na kuwa na maamuzi yenye busara wawapo uwanjni kwenye mashindano muda wote.

 

Kwa kufanya hivyo pia kutaokoa maisha ya mchezaji ambaye amepatwa na matatizo akiwa ndani ya uwanja bila kujali yupo mazingira gani ilimradi naye pia ni mchezaji.

 

Soka sio mchezo wa maumivu bali ni mchezo wa uungwana kwa kila mmoja ndio maana wachezaji wamekuwa wakipeana mikono ikiwa na maana kwamba wote ni kitu kimoja.

 Kwa sasa tunaona kwamba nyota wa Azam FC, Yahya Zayd ambaye ni ingizo jipya kikosini hapo yupo nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita, hata Frank Domayo naye yupo nje kwa ajili ya maumivu aliyopata ndani ya uwanja.

Mbali na huyo hata Simba nahodha wao John Bocco amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara akiwa ndani ya uwanja.

Pia Carlos Calinhos wa Yanga yeye atakosa mechi tatu kwa kuwa alionekana akimpiga ngumi beki wa Ken Gold, Boniphace Mwamnjonde. Haya ni matukio ambayo yanarudisha nyuma maendeleo ya soka letu.

Kumbuka pia hata hivi karibuni Bernard Morrison wa Simba pamoja na Juma Nyoso wa Ruvu Shooting walikutwa na adhabu ya kufungiwa mechi tatu kwa sababu ya kupigana uwanjani.

Ditram Nchimbi naye ndani ya Yanga anamumivu aliyopata kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Ken Gold. Haina maana kwamba wasicheze mpira ama kugongana, jambo la msingi ni tahadhari.

Ukiweka kando wachezaji kujali afya za wengine wimbo mwingine ni kwa waamuzi ambao wanapewa jukumu la kusimamia sheria 17 nao wamekuwa wakionekana kuboronga.


Ligi bora inaendeshwa na waamuzi makini duniani hakuna timu ambayo inaweza kuwa bora kama itakuwa inabebwa ama kufanya vitendo ambavyo vinatoa viashiria vya kubebwa hakuna.


Hivyo waamuzi waache kuchezesha wakichanganya mapenzi yao ya klabu ama maamuzi yao binafsi sio sawa kwa ajili ya afya ya soka.

 

Hili ni doa ambalo linatibua ligi msimu huu na linarejesha nyuma ile morali ya wachezaji pamoja na timu kusaka ushindi.

 

Kila mmoja atimize majukumu yake kwa wakati na kuanza kujipanga ni sasa. Nina imani kupitia ripoti pamoja na yale ambayo yamejitokeza itakuwa ni darasa ili kuwa bora kwa wakati ujao.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments