WAZIRI DKT. NCHEMBA AAGIZA UTEKELEZAJI MPANGO MKAKATI WA MABORESHO ENDELEVU HAKI YA MTOTO NCHINI

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Sifuni Mchome kuhakikisha Mpango Mkakati wa Pili wa Maboresho Endelevu ya Haki Mtoto Nchini unatekelezwa kwa lugha ya kiswahili ili ujumbe uifikie jamii kwa urahisi.

Dkt. Mwigulu Nchemba


Waziri Nchemba aliyasema hayo jana wakati akizindua Mpango Mkakati wa Pili wa Haki Mtoto ambapo alisema utumiaji wa lugha ya Kiswahili katika utekelezaji wa mpango huo utasaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa kwani kila mmoja ataweza kuwajibika kwa nafasi yake kuleta ustawi wa mtoto Nchini.

Alisema Wizara itaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuratibu vyema Mpango huo ikiwemo kuimarisha mfumo wa ulinzi wa mtoto,kuongeza uelewa wa hakinza mtoto katika jamii, kufanyika kwa Maboresho ya sera na Sheria pamoja na kuimarisha uratibu wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mkakati.

 "Lengo la Serikali ni kumlinda mtoto apate haki zake za msingi lakini hili haliwezi kufikiwa ikiwa shughuli zetu tunazifanya kwa lugha za kigeni wakati walengwa ni watanzania Katibu Mkuu hakikisha hili linafanyika kwa lugha ya kiswahili tunajua wananchi wetu waelewe tunatarajia Mkakati huu uwe na matokeo chanya kwa watoto,"alisema Waziri Nchemba.

Aliagiza kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa mpango huo angalau Mara nne kwa mwaka hatua itakayosaidia ufuatiliaji, tathimini na hatua za kuchukua kuboresha pindi changamoto zinapojitokeza huku akiziagiza taasisi kubainisha majukumu yao kuelekea bajeti kuu ya Serikali.

Akizungumzia mafanikio yaliyotokana na Mpango Mkakati wa kwanza alisema uliwezesha kuboreshwa kwa Sheria mbalimbali zinazohusu mtoto ambapo moja ya Sheria iliyorekebishwa ni ya dini inayosema kuingia katika mahusiano ya ndoa ni kosa la ubakaji.

"Nitoe rai kwa taasisi Kujenga uelewa kwa jamii kuhusu haki na wajibu wao kwa mtoto mwaka 2015 ilitungwa Sheria kuhusu vitendo vya ukatili kwa mtoto,uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika vituo vyote vya polisi pamoja na kufanikiwa huku hatutaishia hapa tuna wajibu wa kuwalinda na kuwaandaa wawe raia wema katika Taifa letu na wasimame wenyewe  katika maisha yao,"alieleza Waziri huyo.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania,Shalini Bahuguna aliipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazochukua kulinda haki za mtoto mijini na vijijini.

"Tunaishukuru Sana Serikali kwa kushirikiana na sisi Mashirika mbalimbali na tumeona jitihada zenu kuhakikisha mtoto anakuwa katika mazingira salama na apate haki zake tunategemea Mpango Mkakati huu utakuwa na manufaa na tuko tayari kushirikiana na nyinyi," alisema Mwakilishi Mkaazi huyo. 

Awali akizungumza katika uzinduzi huo Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof.Sifuni Mchome alieleza baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo alisema ni pamoja na Uchache wa wataalamu wa masuala ya watoto, Taasisi kutotenga bajeti,baadhi ya magereza kukosa sehemu maalumu  kwa ajili ya watoto.

"Harakati za kufanikisha usalama wa mtoto zinaendela kwani maafisa 638 kutoka Kanda 14 wanaendesha kesi za watoto walijengewa uwezo,huduma za msaada wa kisheria zimeongezeka,mahakama za watoto zimeongeza kutoka moja hadi 130 

Aidha, mmoja wa wadau walioshiriki katika uzinduzi huo Fatuma Abdalah Mwakilishi kutoka Time ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUT) alisema tume hiyo imeanzisha mfumo wa mtandao utakaosaidia wananchi kutoa malalamiko yao ili kuwafikia wengi zaidi na kulinda utu wa mtoto.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments