YANGA WATAJA MAMBO ALIYOWATENDEA RAIS JOHN MAGUFULI


 WAKATI taifa likiwa kwenye majonzi mazito na maombolezo ya siku 21 ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, Klabu ya Yanga imetaja mambo matatu mazuri aliyowafanyia katika utawala wake.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Rais Magufuli afariki dunia kabla ya Rais Mama Samia Hassan Suluhu kuapishwa Ikulu ya Dar es Salaam. Rais Magufuli alifariki Jumatano Machi 17, jioni kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena Dar.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Kaimu Katibu Mkuu, CPA Haji Mfikirwa pamoja na kutoa salam za Rambirambi alisema chini ya uongozi wa Rais Magufuli nchi imepiga hatua kwenye sekta ya michezo.

 

Mfikirwa alisema kuwa kwa upande wao Yanga Rais Magufuli ameifanyia mengi makubwa klabu hiyo na kati ya hayo yapo matatu ambayo hawatayasahau ambayo ni;“Moja, alitaka kuiona michezo iwe ya kisasa ili tuweze kushindana na klabu kubwa barani Afrika kupitia hotuba zake alizokuwa akizitoa Rais Magufuli ambayo ilitutaka kuingia kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa klabu na sisi kama Yanga ndiyo tunaenda nayo.

 

“Pili, alitusaidia kuziba mianya ya dhuluma kwa klabu, awali mapato ya klabu na serikali yaliyopotea sana, lakini alituletea mfumo wa N-Cards ambao klabu sasa hivi zinapata mapato yake halali viwanjani.

 

"Tatu, alikuwa rais wa bahati kwa Yanga, kwani katika mechi zetu alizohudhuria mara zote tulishinda. Nakumbuka alikuja kwenye Dabi ya Kariakoo na tukashinda bao 1-0 ambalo lilifungwa na Morison (Bernard), hivyo kwetu alikuwa rais wa bahati sana.


"Kutokana na kuwa na mafanikio kwetu, na dhamira yetu msimu huu ni kutwaa ubingwa, iwapo tutafanikiwa kuuchukua, basi ubingwa tutautoa kama zawadi kwake katika kumkumbuka Rais Magufuli.

 

“Na mwisho, kwa niaba ya uongozi niombe bendera zote za klabu yetu kuanzia hapa makao makuu na matawi yote nchini, bendera zote zipepee nusu mlingoti kipindi hiki cha maombolezo ya kifo cha kipenzi chetu, Rais Magufuli kwa muda uliotangazwa na Serikali,” amesema Mfikirwa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments