Recent-Post

Hifadhi ya Gombe yatoa Sh981 milioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo vijijini


Kigoma. Hifadhi ya Taifa ya Gombe imetumia karibu Sh1 bilioni kusaidia jamii zinazopakana na hifadhi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza jana Aprili 26 katika hifadhi hiyo, mkuu wa idara ya uhusiano ya jamii, Nelson Mcharo amesema Sh981milioni zimetumika katika kusaidia jamii ikiwemo ujenzi wa madarasa 22, nyumba za watumishi nane,ofisi za shule tano,  ujenzi wa kituo cha Polisi na mabweni mawili, vyoo vya shule, maktaba moja na kutoa madawati 240.

Mbali ya ujenzi wa majengo hayo, pia amesema wamesaidia miradi ya ujasiriamali kwa lengo la wananchi kujikwamua kiuchumi na  kuachana na ujangili katika kujipatia kipato kwa kusaidia ufugaji nyuki na ng'ombe wa maziwa.

Kupitia njia hii wananchi hunufaika moja kwa moja na uwepo wa hifadhi katika maeneo yao na hivyo kushiriki moja kwa moja katika kuilinda hifadhi," amesema Mcharo.

Mcharo amesema wametoa elimu kwa wananchi wanaozunguka hifadhi kuhusu utunzaji mazingira wakitumia mikutano, kuwezesha makundi mbalimbali kutembelea hifadhi na sinema zinazoelimisha kuhusu uhifadhi.

Kwa upande wa ajira, amesema jumla ya ajira 26 zimetolewa,mbili zikiwa za kudumu na 24 zisizo za kudumu.
Naye ofisa mhifadhi daraja la pili, Iddi Kaluse amesema watalii wanaotaka kwenda hifadhi ya Gombe, hupenda kufahamu usafiri watakaotumia ambao ni usafiri wa majini.

Post a Comment

0 Comments