Hata hivyo, wamesema hotuba yake hiyo haikugusia mambo muhimu ambayo yamekuwa yakiibua mjadala katika jamii, likiwamo suala la kubadilisha sheria kandamizi na kutengeneza Katiba mpya.
Katika hotuba yake aliyoitoa bungeni juzi, Rais Samia alisema anakusudia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini, ili kuweka mwelekeo wa namna ya kuendesha shughuli za siasa zenye tija na masilahi kwa Taifa.
Akizungumzia hotuba ya Rais Samia, Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kamati kuu ya NCCR-Mageuzi, imetoa mapendekezo manne kwa Serikali ya awamu ya sita, ikiwamo kuunda tume ya suluhu na maridhiano ili kupata mwafaka wa kitaifa.
Mbatia alisisitiza kuwa hatatarajia kusikia chombo chochote kilichopo serikalini, likiwamo jeshi la polisi linazuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara kwa kuwa ni haki yao kikatiba.
“Rais ametoa rai atakutana na vyama vya siasa, ni jambo la heri, lakini hatusubiri hadi tukutane na Rais Samia ndio tukafanye mikutano yetu, ni matakwa ya kikatiba na ni haki yetu,” alisisitiza.
0 Comments