Recent-Post

Wazazi wanatakiwa kulinda maslahi na haki za watoto

Halmashauri ya Wilaya ya kigamboni imesema wazazi wanajukumu la kukaa pamoja na watoto kuhakikisha maslahi na haki zao za msingi  zinalindwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya maisha yao.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Juni 16, 2021 na Katibu tawala wa  Wilaya hiyo,Dalmia Mikaya ikiwa ni  kilele cha maadhimisho siku ya watoto wa Afrika, yenye kauli mbiu ya ‘Tutekeleze ajenda 2040: kwa Afrika inayolinda haki za watoto’.

Amesema watoto wanapitia changamoto mbalimbali ikiwemo kunyanyaswa, kupata mimba na  kutumia madawa ya kulevya vitendo ambayo vinashusha utu na hadhi yao katika jamii..

Amesema jamii yote inayowazunguka ikiongozwa na wazazi wanalojukumu la kuungana kupinga vitendo vibaya na kuwalea watoto kwenye maadili yanayotakiwa kwa kuhakikisha wanapata elimu.

"Niwaombe wazazi na jamii kwa ujumla wakati tunaadhimisha siku hii ni fursa kwetu kuwalinda watoto wetu dhidi ya ukatili wanaofanyiwa na kuhakikisha wanatambua haki zao"amesema

Naye Diwani wa Kata ya Mji Mwema,  Omary Ngurangwa amesema Jamii inatakiwa kutoa mabalozi wazuri wa kulinda haki zao na serikali inapaswa kushirikiana na wadau kuona umuhimu wa kuilinda jamii.

ADVERTISEMENT

"kuna watoto wengi wanafanyishwa kazi za ndani na waasa kuwa mabalozi wazuri kulinda haki za watoto,"amesema

Naye Meneja wa Baraza la taifa la watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (NACOPHA) kwa Kanda ya Dar es Salaam, Victoria  Huburys amesema  wanathamini na kutambua umuhimu wa watoto katika maendeleo ya jamii.
"Mtoto anatakiwa kuishi na kupata afya njema na bora ili anufaike, Afrika inataka kila mtoto anayezaliwa anapata haki na tupo hapa kushirikiana na serikali kutambua umuhimu wa watoto katika jamii,"amesema Victoria

Maadhimisho hayo yaliyoasisiwa mwaka 1991 na umoja wa Afrika (OAU) yanafanyika kila mwaka ikiwa ni kumbukizi ya mauaji ya kikatili walivyofanyiwa watoto wa kijiji cha Soweto Afrika Kusini mwaka 1976.

Post a Comment

0 Comments