Bosi GSM amchangia Mdamu Sh6 millioni

Mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni Rais wa Kampuni ya GSM, Ghalib Said Mohamed, ametoa  Sh6  milioni mchango wa matibabu ya mchezaji wa Polisi Tanzania, Gerard Mathias Mdamu.

 Mdamu alivunjika miguu yote miwili Julai 9, wakati kikosi hicho kilipopata ajali mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro, kitokea mazoezini Uwanja wa TPC.

Timu hiyo ilikuwa ikielekea kambini kwa ajili ya kumalizia mechi za mwisho za msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21.

Akifanya mahojiano na kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM leo, msemaji mpya wa Yanga, Haji Manara amesema Ghalib ameguswa na tukio hilo la Gerard kupata majeraha hivyo kuamua kutoa kiasi hicho cha fedha ambacho kitamsaidia katika matibabu yake.

Ghalib ni mtu wa watu na kama wengine walivyojitokeza kumchangia mchezaji huyo wa Polisi Tanzania nae pia ameguswa na kutoa mchango wake ambapo tutaukabidhi sehemu husika," alisema Manara ambaye ni msemaji wa zamani wa Simba.

Naye Haji Manara kwa upande wake amechangia kiasi cha dola za kimarekani 300 na sh10,000 ya kitanzania kwa ujumla ni sh700,000 kwa ajili ya matibabu ya mchezaji huyo aliyelazwa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Natoa laki saba ambayo ni mshahara wangu wa mwezi wa saba kama sehemu ya kumchangia Mdamu ambaye sote kwa ujumla tunajua hali anayopitia," alisema Manara.

Katika hatua nyingine Manara alisema wao kama viongozi wa Yanga wataendelea kumchangia Mdamu ili kuhakikisha anapona na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Huu ni mwanzo tu ila malengo yetu kama Yanga kwa ujumla ni kumsaidia Mdamu kupata matibabu zaidi ili tumuone akirejea kwenye majukumu yake ya kila siku kama walivyo watu wengine," alisema.

Wadau mbalimbali wa michezo nchini wamekuwa wakiguswa na kumchangia Mchezaji huyo huku wengi wao wakiandaa mechi za hisani ili tu kuhakikisha wanapata fedha kumsaidia katika matibabu yake.

Mdamu anaendelea kupatiwa matibabu ambapo leo alhamisi anatarajiwa kufanyiwa operesheni kwenye miguu yake yote miwili iliyovunjika. Mwananchi juzi lilishuhudia mchezaji huyo akilia kitandani kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo miguuni kwenye vidonda vibichi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments