JOHN BOCCO, MZAWA ALIYEVUNJA UFALME WA WAGENI

Akiwa ni mzawa namba moja kwa kucheka na nyavu na kinara kwa wacheka nyavu kwa msimu wa 2020/21 ndani ya Ligi Kuu Bara, John Bocco amekuwa na wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 78.

Rekodi zinaonyesha kuwa kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes kikiwa kimecheza jumla ya mechi 34 ni mechi 23 pekee nyota huyo aliweza kucheza.

Licha ya kucheza mechi hizo bado alishuhudia timu hiyo ikiweza kutetea taji lake la Ligi Kuu Bara kwa kufikisha jumla ya pointi 83 na walifunga jumla ya mabao 78 huku mzawa huyo akivunja ule ufalme wa wageni Bongo.

Katika mechi hizo 34 ambazo ni sawa na dakika 3,060 Bocco aliyeyusha jumla ya dakika 1,249 ndani ya uwanja kwenye mechi za Ligi Kuu Bara pekee.

Ni mechi 6 pekee Bocco aliyeyusha dakika 90 na kumfanya atumie dakika 540 jumlajumla huku mechi  17 akikwama kuyeyusha dakika 90 mazima ndani ya uwanja.Alikosekana kwenye mechi 11 za ligi ambazo ni sawa na dakika 990.

Katika dakika hizo ambazo alitumia Bocco aliweza kutupia jumla ya mabao 16 na kuwa ni kinara kwa msimu wa 2020/21 akiwa ni mzawa ambaye aliweza kuwa bora kwenye eneo la ushambuliaji na kuuvunja ule utawala wa Meddie Kagere ambao ulitawala kwa misimu miwili mfululizo.

Kagere ambaye ni raia wa Rwanda yeye yupo ndani ya Simba aliweza kuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo alianza msimu wake wa kwanza wa 2018/19 alipotupia mabao 23 na ule wa 2019/20 alipotupia mabao 22.

Mzawa Bocco pia katika mabao yake hayo 16 anakumbuka kwamba alisepa na mpira wake mmoja ambao upo kabatini kwa kuwa alifunga hat trick moja ilikuwa mbele ya Coastal Union wakati timu yake ikishinda mabao 7-0. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments