Recent-Post

Serikali yamwekea pingamizi Mbowe kesi aliyofungua

 

Serikali imemwekea pingamizi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katika kesi yake kikatiba, ikitaja sababu nne na kudai kuwa kesi hiyo ni batili kwa kuwa ina upungufu wa kisheria.

Hivyo Serikali inaiomba mahakama hiyo iifute kesi hiyo bila kuisikiliza hoja za msingi.

Mbowe alifungua kesi hiyo ya kikatiba Julai 30 mwaka huu, Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika kesi hiyo namba 21 ya mwaka 2021, Mbowe anapinga utaratubu uliotumika kumkamata, kumweka kizuizini na hatimaye kumfungulia kesi ya uhujumu uchumi akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Soma hapa: Mashahidi 24 vielelezo 19 kesi ya Mbowe na wenzake

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji John Mgetta, akishirikiana na Jaji Leila Mgonya na Jaji Stephen Magoiga, ilitajwa kwa mara ya kwanza Agosti 9, mwakaha huu ambapo waidai waliomba siku 14 kuwasilisha majibu yao dhidi ya madai ya Mbowe.

Leo Agosti 30, kiongozi wa jopo la wadaiwa, wakili wa Serikali Mkuu Hangi Chang’a amekanusha madai ya Mbowe.
Wakili Kibatala kwa upande wake aliieleza mahakama kuwa baada ya kurejea mambo mbalimbali kushusiana na kesi hiy wameona kwamba hakuna haja ya kuwasilisha kiapo cha ziada.

Kutokana na pingamizi hilo la awali, kama ilivyo kawaida, mahakama imelazimika kusimamisha kwanza mwenendo wa kesi ya msingi na badala yake itasikiliza na kuamua kwanza pingamizi la Serikali.

Soma hapa: Ole Sabaya, IGP Sirro kuwa mashahidi kesi ya Mbowe

Ikiwa mahakama itakubaliana na hoja za pingamizi la Serikali, basi itaitupilia mbali kesi hiyo na hicho ndicho kitakuwa kifo chake.

Lakini kama mahakama itupilia mbali hoja za pingamizi la Serikali basi kesi hiyo itakwenda katika hatua ya pili ambayo ni usikilizwaji wa hoja za Mbowe katika kesi ya msingi pamoja na hoja za Serikali kuhusiana na madaia ya Mbowe na kisha itatoa uamuzi.

Katika usikilizwaji wa pingamizi hilo la awali, Wakili Chang’a aliomba ufanyike kwa njia ya maandishi maombi ambayo mahakama imekubaliana nayo baada ya mawakili wa Mbowe kueleza kuwa hawana pingamizi dhidi ya maombi ya Serikali ya kusikiliza pingamizi hilo kwa njia ya maandishi.

Soma hapa:Marekani yajitosa kesi ya Mbowe

Jaji Mgetta ambaye atasikiliza na kuama pingamizi hilo aliwataka Serikali kuwasilisha hoja zake za maandishi Septemba 6 na Mbowe kuwasilisha majibu yake ya hoja za pingamizi la Serikali Septemba 9 mwaka huu.

Pia Jaji Mgetta aliiamuru Serikali kama itakuwa na hoja za nyongeza kuhusu majibu ya Mbowe, kuziwasilisha mahakamani Septemba 13 na akapanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Septemba 23, mwaka huu, saa Nane Mchana.

Imeandikwa na Glorian Sulle na Rukia Kiswamba

Post a Comment

0 Comments