Uamuzi kesi ya ugaidi dhidi ya Mbowe leo

             

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, leo Jumatano Septemba 1, 2021 inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anayetaka imwachie huru kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya ugaidi dhidi yake.

Mbowe, anayekabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi na ugaidi, amekuwa rumande kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa akisubiri hatima yake.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alikamatwa Julai jijini Mwanza pamoja na wanachama wengine 10 walipokuwa wakijiandaa kufanya kongamano la kushinikiza kupatikana kwa Katiba Mpya nchini.

Mbowe alisafirishwa hadi Dar es Salaam kabla ya kushtakiwa na wenzake wawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.

Awali, kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji mbele ya Jaji Elinazer Luvanda, lakini ilipoitwa jana, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando aliieleza Mahakama kuwa walipokea pingamizi kutoka kwa mawakili wa Mbowe kuhusu mamlaka ya Mahakama na kuomba mwongozo.

Wakili wa Mbowe na wenzake, Peter Kibatala aliieleza Mahakama kuwa wateja wake wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, Mahakama hiyo imetengwa maalumu kwa ajili ya kusikiliza makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, hivyo inakosa mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya ugaidi dhidi ya wateja wao.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments