YANGA HAWAPOI, WAIDUKUA MECHI YA SIMBA YOTE

 


YANGA imefanya umafia huko nchini Morocco baada ya kudukua mtandaoni linki ya mchezo wa kirafiki wa Simba na kuungalia wote, huku wakisema mabao hayakuwa halali.

 

Simba Jumamosi ilicheza mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya AS Rabbat ya nchini Morocco ambako timu hiyo imeweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu ujao na kumaliza kwa sare ya mabao 2-2, huku mabao ya Simba yakifungwa na Ousmane Sakho na Hassani Dilunga.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo waliutazama mchezo wote pamoja na kwamba ulipigwa pini usionyeshwe.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, walipanga kuwatuma mashushushu kwenda kuutazama mchezo  huo, lakini kutokana na umbali wa mji ambao Simba wamefikia huko Rabbat, walishindwa lakini wakawatumia watu wa pale pale kuwapa linki.

 

Aliongeza kuwa kutoka Marrakech ambako wamefikia kwenda Rabbat ni mwendo wa saa nane kwa kutumia gari, hivyo wakawatumia wataalam wao mitandao kwa ajili ya kudukua linki ya mchezo huo ambao ulikuwa ukionyeshwa mtandaoni kwenye mji husika tu.

 

“Tulipanga muda mrefu kwenda kuwatazama Simba wakicheza mchezo wake wa kirafiki kwa lengo kuwajua wachezaji wapya waliowasajili pamoja na kuujua ubora wa timu yao.

 

“Lakini ilishindikana kutokana na umbali uliopo kutoka katika mji tuliokuwa ambao Marrakech kwenda Rabbat hapa Morocco walipofikia Simba.

 

“Licha ya kushindwa kwenda huko, lakini tumefanikiwa malengo yetu baada ya kocha na wachezaji kufanikiwa kuwaangalia Simba kwa kupitia mtandaoni, baada ya kuidukua linki ya mchezo huo.

 

“Kocha ameona ubora na upungufu wao, na kikubwa Simba wenyewe mabao yenyewe ambayo wamefunga yote yalikuwa ya kuotea (offside),” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Akithibitisha hilo Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema kuwa “Tumeuona mchezo wa kirafiki ambao Simba wameucheza kupitia mtandaoni, hivyo tumeona upungufu na ubora wao, kikubwa tukutane katika msimu ujao ambao tumepanga kufanya mengi makubwa.”

 

Taarifa zinasema kuwa wakati mchezo unaendelea kuna mtu wa upande wa Yanga alikuwa pale uwanjani na ndiye alifanya kazi kubwa hakikikisha mechi wanaiona.

24Aug2021

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments