Achana na matokeo ya kikosi Cha Yanga kukubali kipigo cha 2-1 kiwango cha baadhi ya nyota wao kimesababisha mashabiki wa Yanga kujitapa kuwa hata kesho tu ligi ianze na ubingwa wanachukua.
Licha ya kufungwa mabao 2-1 na Zanaco katika mechi ya kirafiki Jana lakini hilo Wala halikuwasumbua mashabiki wa Yanga ambao wamekubali matokeo na kusema kuwa kwenye ligi moto utawaka.
Bao maridadi lililofungwa na mshambuliaji Heritier Makambo dakika ya 37 lilitosha kuwapa jeuri mashabiki wa Yanga ambao walikuwa wakishangilia kwa staili ya kuwajaza huku wakitamba kuwa msimu ujao wapinzani wao mbona wataomba poo.
Makambo alifunga bao hilo baada ya kuwachambua mabeki wawili wa Zanaco na kisha kuachia shuti Kali na kumuacha kipa wa Racha Kola akishangaa.
Makambo ambaye aliwahi kuichezea Yanga msimu wa 2018/2019 alionyesha kiwango kizuri licha ya kukosa mabao kadhaa baada ya kubanwa na mabeki wa Zanaco.
Yanga ilianza mchezo huo kwa Kasi na dakika ya kwanza tu tayari walishafika golini kwa wapinzami wao lakini mabeki wa Zanaco walikuwa imara kuokoa hatati zote.
Dakika ya 7,Djuma Shaban aliambaa na mpira na kupiga krosi safi iliyounganishwa kwa kichwa na Makambo na mpira kutoka nje.
Dakika ya nane krosi ya Farid Mussa ilikosa mmaliziaji na kuokolewa na mabeki wa Zanaco.
Yanga iliendelea kukiandama lango la Zanaco ambapo dakika ya 12, Jesus Moloko alipiga krosi nzuri iliyodakwa na kipa wa Zanaco, Racha.
Dakika ya 14 nusura Feisal Salum aipatie Yanga bao kama si juhudi za kipa wa wapinzami wao kupangua shuti lililopigwa na kiungo huyo.
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra alifanga kazi ya zoada dakika ya 25 baada ya kudaka shuti la mshambuliaji wa Zanaco, Evance Katema ambaye aliwachambua mabeki wawili wa Yanga, Kibwana Shomari na Bakari Mwamnyeto na kupiga shuti la kawaida lililodakwa na kipa huyo raia wa Mali na kuamsha shangwe uwanjani hapo.
Kipindi Cha pili wachezaji wa Yanga waliiingia wakiwa wamevaa jezi mpya za Njano tofauti na kipindi Cha kwanza walipongia na jezi za Kijani na kuanza mpira taratibu tofauti na walivyoanza kipindi Cha kwanza.
Kipindi hicho cha pili Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mukoko Tonombe na Makambo na kuwaingiza Yanick Bangala na Fiston Mayele.
Dakika chache tu baada ya mabadiliko hayo , Zanaco ilipata bao la kusawazisha dakika ya 61 kupitia kwa Akim Mwemba kwa shuti la kawaida akimalizia mpira wa Kona.
Yanga iliendelea kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Djuma Shaban, Feisal Salum, Farid Mussa na Jesus Moloko na kuwaingiza Paul Godrey ,Said Ntibazonkiza, Dickson Ambundo na Yacouba Sogne.
Mabadiliko hayo hayakuonekana kuwasaidia Yanga kwani ni kama walipooza na kucheza soka la taratibu kama la wapinzani wao.
Dakika ya 77 Zanaco walipata bao la pili lililofungwa na John Sinombo na kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kuishangilia kwa staili ya kuwajaza.
Djuma,Mokolo ni moto
Kama kuna wachezaji waliowakosha mashabiki wa Yanga katika mchezo wa Jana basi ni beki wa kushoto, Djuma Shaban na winga,Jesus Moloko.
Wachezaji hao kutoka DR Congo walionyesha kiwango kizuri na kuamsha shangwe Kila mara kutoka kwa mashabiki.
Djuma alionekana kuwa na kasi na kuipandisha timu mbele huku akitoa krosi nzuri kwa washambuliaji wa Yanga ambao kama wangekuwa makini wangeweza kupata mabao mengine zaidi.
Kwa upande wa Moloko alionekana kuwa mwiba kwa mabeki wa Zanaco huku akiwakosha watu wengi kutokana na jinsi anavyojua kuficha mpira mguuni kwake na uwezo wa kuwachambua mabeki wa timu pinzani.
0 Comments