AJALI YA HIACE, TREKTA YAUA NA KUJERUHI 7 SHINYANGA


Gari yenye namba T.470 DEL aina ya Hiace, mali ya Kisimbo & Son Ltd baada ya kupata ajali

Mwanaume mmoja amefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya gari yenye namba T. 470 DEL aina ya Hiace, mali ya Kisimbo & Son Ltd kugonga Trekta katika kijiji cha Ishinabulandi kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga kwenye barabara ya Tinde – Tabora.
Ajali hiyo imetokea jana Jumatatu Septemba 13,2021 majira ya saa mbili na nusu usiku katika barabara ya Tinde kuelekea Tabora.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema ajali hiyo imehusisha gari yenye namba T.470 DEL aina ya Hiace, mali ya Kisimbo & Son Ltd ikiendeshwa na Sudi Ntawigaya mwenye umri kati ya miaka 25-30 ,mkazi wa Ibinzamata Mjini Shinyanga kugonga Trekta lenye namba T.623 CKY na tela lenye namba T.166 CGU likiendeshwa Shija Steven mkazi wa Ishinabulandi wilayani Shinyanga.

"Ajali hiyo ilisababisha kifo kwa abiria mmoja asiyefahamika jina, umri wala makazi, na majeruhi kwa abiria saba wakazi wa Shinyanga ambao wamelazwa wanaendea na matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga",amesema.

Amewataja majeruhi hao kuwa ni Shija Deus (20) mkazi wa kijiji cha Ishinaublandi,amepasuka kichwa, Mohamed Juma (21) mkazi wa Ishinabulandi amepasuka kichwa pamoja na mdomo na mkono wa kushoto umevunjika na Venance Jonas (31) mkazi wa Ndala, kichwa kimepasuka,mkono wa kushoto umevunjika.

“Majeruhi wengine ni Maneno Charles (27) mkazi wa Kitangili ameumia kichwani na kuvunjika mkono wa kulia, Paulo Stephano (26) amevunjika mkono wa kulia,Shabani Mohamed (35) mkazi wa Majengo Mapya, ameumia shingo na kuvunjika mkono wa kulia na Josia Magabe, (33) makazi wa Kitangili”,ameongeza.

Kamanda Kyando amesema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Hiece kutaka kuyapita magari mengine kwa mwendo hatarishi.

"Dereva wa Hiace amekimbia mara tu baada ya kusababisha ajali. Juhudi za kumtafuta zinaendelea na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga",amesema.
Na Kadama Malunde 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments