Recent-Post

Aliyekaa mochwari miezi minane azikwa

Hatimaye mwili wa Mzee Wilson Ogeta (89) umezikwa kijijini Nyambogo baada ya kukaa mochwari takriban miezi minane bila kuzikwa, kufuatia mgogoro wa ardhi kati ya familia ya mzee huyo na mtu mmoja anayedaiwa kununua eneo la makazi ya mzee huyo.

Mzee Wilson Ogeta alifariki dunia Januari 10 mwaka huu, lakini mwili wake haukuzikwa hadi juzi kutokana na kuwepo kwa mgogoro wa umiliki wa ardhi kati yake na mtu mmoja anayedaiwa kununua eneo hilo.

Mazishi hayo yamefanyika juzi, ikiwa ni jitihada za Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka kuingilia kati mgogoro huo wa umiliki wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka sita sasa na wahusika kushindwa kufikia suluhu.

Mkuu wa wilaya ya Rorya ndiye aliyeongoza wakazi wa kijiji cha Nyambogo na vijiji jirani waliojitokeza kushuhudia mazishi hayo ya aina yake kutokana na marehemu kukaa muda mrefu bila kuzikwa.

Akizungumza msibani hapo, Chikoka alisema kuwa utu wa mtu ni jambo la msingi sana na kwamba baada ya kupata taarifa juu ya uwepo wa mwili huo mochwari kwa miezi minane, aliamua kuwa kabla ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo ni vema mwili ukazikwa kwanza.

Alisema Serikali imegharimia mazishi na hifadhi ya mwili huo kuanzia Januari hadi alipozikwa juzi.

Alisema kuwa wamekubaliana pande zote zikutane Septemba 7 ofisini kwake kwa majadiliano zaidi, huku akiagiza mtu anayedaiwa kuuza eneo hilo bila kushirikisha familia naye awepo.

Mtoto wa marehemu, Samson Wilson alimshukuru Chikoka kwa jitihada alizofanya hadi baba yao amezikwa baada ya familia kuhangaika kwa muda mrefu.

Post a Comment

0 Comments