Recent-Post

BIASHARA UNITED, AZAM FC MAMBO SAFI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKANa Mwandishi Wetu, Michuzi TV

MICHUANO ya ngazi za vilabu ya Kombe la Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF Confederation Cup) msimu wa 2021-2022 rasmi yamenza kutimua vumbi huku wawakilishi wa Tanzania katika Michuano hiyo, Biashara United na Azam FC wakianza vyema michezo yao ya hatua za awali ya michuano hiyo.

Biashara United ya Mara imeanza vyema Michuano hiyo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji wao, FC Dikhil ya Djibouti katika mchezo uliopigwa nchini humo siku ya Ijumaa, bao pekee la Wanajeshi wa Mpakani likifungwa na Winga machachari, Dennis Nkane katika dakika ya 52 ya mchezo huo.

Matokeo hayo ya bao 1-0 ugenini, ni matokeo bora na mazuri kwa Biashara kutokana na ugeni wao katika mashindano ya Kimataifa wakishiriki kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa timu yao na kupanda Ligi Kuu Soka nchini Tanzania. Mchezo wa marudiano utachezwa nchini Tanzania baada ya wiki moja Biashara wakiwa nyumbani.

Azam FC wao wamepata ushindi wa bao 3-1 dhidi ya wageni Horseed FC kutoka Somalia mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam, huku mabao ya Azam yakifungwa na Ayoub Lyanga dakika ya 32, bao la pili limefungwa na Idriss Mbombo dakika ya 73 na la tatu likiwekwa kambani na Beki Lusajo Mwaikenda dakika ya 78, bao la Horseed limefungwa na Ibrahim Nor kwa faulo safi dakik ya 23 ya mchezo.

Mchezo wa pili utachezwa hapa hapa Dar es Salaam katika uwanja wa Uhuru wiki moja baadae kati ya Septemba 18-19, 2021 wakati Horseed FC kutoka Somalia wakiwa wenyeji katika uwanja huo.


Post a Comment

0 Comments