Binkleb atamba wenye Yanga yao wamerudi


 YANGA imesuka kamati ya vichwa 9 ambayo rekodi zao zinaonyesha mara ya mwisho wakiwa pamoja Yanga ilibeba ndoo mara nne mfululizo kama ilivyo kwa Simba sasa,huku Abdallah Binkleb akisisitiza kwamba ; “sasa ni kazi tu.”

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msola amesuka kamati hiyo ya utendaji itakayoongozwa na mwenyekiti Rodgers Gumbo akiwa na watu tisa ambao ni Hamad Islam, Lucas Mashauri, Abdallah Binkleb, Mhandisi Hersi Said,Seif Ahmed ‘Seif Magari’, Arafat Haji,Davis Mosha na Pelegrinius Rutayunga.

Katika kamati hiyo kuna watu sita ambao wamewahi kukutana kwenye kamati hiyo ambao wakati huo Yanga haikupishana na taji la Ligi mpaka walipojiweka pembeni kwasababu mbalimbali.

Bin Kleb,Seif Magari wamewahi kuongoza kamati hiyo kwa nyakati tofauti katika uongozi wa bilionea Yusuf Manji,Lloyd Nchunga lakini pia wamewahi kukutana na Mosha, Mashauri,Islam,Gumbo katika majukumu ya kamati hiyo pamoja na ile ya usajili enzi hizo Yanga ikiwa tishio zaidi.

Katika enzi vigogo hao wakiiongoza Yanga ilichukua mataji mara nne kwa nyakati tofauti katika misimu ya ya 2012/13,2014/15,2015/16 kisha wakamalizia msimu wa mwisho Yanga kuwa bingwa 2016/17.

Baada ya miaka hiyo Yanga haikuwahi kuambulia taji lolote. Msimu uliopita walichukua taji la Mapinduzi kule Zanzibar huku watani wao Simba wakichukua ubingwa wa Bara mara nne mfululizo na mataji mengine kibao.

Vigogo hao sasa wanarudi tena safari hii na kete yao ya kwanza itakuwa msimu ujao wakiungana na sura nyingine mpya wakiwemo Hersi,Arafat na Rutayuga.

Mtihani wao wa kwanza ni michuano ya kimataifa Yanga ikivaa na River United Septemba 12 Jijini Dar es Salaam kisha marudiano ugenini halafu watawakabili Simba kwenye ngao ya jamii.


BINKLEB

Baada ya kumkosa Gumbo jana Mwanaspoti lilimpata Binkleb akasema; “Hili sio jukumu rahisi ni kazi nzito,nimekuwa katika kamati hizi kwa miaka mingi najua kazi zake, Yanga imekosa ubingwa kwa miaka mingi na kila mmoja anayeipenda klabu hii anatamani kuona hilo na sasa imani hiyo itaongezweka kutokana na uwepo wetu,”alisema Binkleb.

“Jambo la kushukuru wadhamini wetu GSM na uongozi wa klabu wametengeneza timu ambayo tunaona ina sura ya ubora na kupigania mataji ingawa bado tunatakiwa kuipa muda ikae sawasawa kiushindani.

“Sisi kama kamati ni kama viongozi tu tunaochora ramani lakini uwepo wetu hautakuwa na maana kama wanachama wengine watakaa chini na kunyoosha miguu wasiposhirikiana nasi katika kuipigania timu yetu,naamini wanaofurahia uwepo wetu nao wanatakiwa kuingia vitani kama sisi tutakavyokuwa tunaisimamia timu.

“Ligi itakuwa ngumu msimu ujao,nafurahi kuona kuna udhamini mkubwa wa Azam media wenye nguvu ambao sasa utaifanya kila timu kupigania nafasi yake ili wapate kitu mwisho wa msimu, hakutakuwa na timu zitakazojilegeza kuachia timu zingine.

“Kazi yetu ni kusimamia Yanga iwe bora kiwanjani na sio kitu kingine hilo naamini kwa nguvu yetu na wadhamini pamoja na klabu ka ujumla linawezekana kutokana na ubora wa timu yetu.”

Naye Mashauri ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa kamati maalum katika mpito wa kusaka uongozi mpya kabla ya kuingia Msola alisema; “Huwezi kukataa kila wakati kupokea majukumu ya kuisaidia klabu unayoipenda,tunafahamu ni kazi ngumu lakini kwanza lazima tuwaheshimu wenzetu ambao walituita na kuona tuna kitu cha kuiwasaidia.”

“Tutakutana na mwenyekiti wetu wa kamati,uongozi wa klabu na hata mdhamini Ghalib (Said) ambaye ametupa heshima hii tutajadiliana juu ya malengo ya klabu na hayo ndio tunayokwenda kuyasimamia,”alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments