CCM yatangaza kuingia kwenye uchaguzi mdogo jimbo la Konde

 

Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (Nec) ikitangaza uchaguzi wa marudio jimbo la Konde kufanyika Oktoba 9 mwaka huu, CCM) imesema imejipanga kushiriki uchaguzi huo na itaibuka kidedea.

Uchaguzi huo unafanyika ikiwa ni baada ya aliyechaguliwa Julai 18, 2021 kupitia chama hicho, Sheha Faki Mpemba kujiuzulu nafasi hiyo kabla ya kuapishwa kutokana na kile alichodai ni matatizo ya kifamilia.

Zaidi, Mpemba alieleza kuwa anatishiwa maisha na watu aliodai ni wapinzani wake wa kisiasa hivyo familia ikamshauri aachie ngazi kwa ajili ya usalama wake na familia pia.

Hata hivyo, baadaye Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud alisema kwamba Faki alijiuzulu kwasababu chama cha ACT - Wazalendo kilipeleka malamiko yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein  Mwinyi jinsi kilivyodhulumiwa katika uchaguzi huo hivyo kuamua busara itendeke ili kulinda maslahi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mustakabali wa Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Septemba 6, 2021 ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja, Katibu wa Kamati maalumu, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Nao amesema chama kimejipanga vyema kushiriki uchaguzi huo.

“Tunakwenda Konde. Tumekaa kamati maalumu jana tumeanza mchakato kutoka kwenye kamati ya siasa ya wilaya na mkoa, kwahiyo tunakwenda kwenye kamati kuu keshokutwa kwa ajili ya kumpata mgombea. Tunakwenda kufanya uchaguzi wa kistaarabu usiokuwa na mashaka, namimi nasema CCM itaibuka kidedea,”

Wakati huohuo Nao amesema kamati kuu ya chama hicho imeridhishwa na utendaji kazi wa viongozi wa kitaifa Rais Samia na Dk Mwinyi kwa utendaji kazi wao uliotukuka.

Amesema; “CCM tumeridhika na jinsi viongozi hawa wanavyochapa kazi mambo yanayofanywa ni makubwa na yanaleta matumaini makubwa.

Amesema Rais Samia amesikiliza kilio cha wananchi kuhusu tozo za miamala ya simu na kupuguza kiwango cha makato huku Dk mwinyi akiendelea kushughulikia watendaji wabadhirifu wa mali za umma tatizo ambalo lilikuwa limeota mizizi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments