DC Lushoto atoa miezi mitatu halmashauri kumaliza jengo la mama na mtoto

 MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro ameipa miezi mitatu Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto iwe imekamilisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto linalojengwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.

Lazaro ambaye alifika kwenye jengo hilo Septemba 27, 2021 ikiwa ni sehemu ya kukagua miradi ya maendeleo, alisema umefika wakati sasa wa kukamilisha jengo hilo baada ya kukaa mwaka mzima, huku akisema jengo hilo ambalo Serikali Kuu imetoa sh. milioni 400, lakini bado limeshindwa kukamilka kwa wakati, ni hasara kwa Serikali na wananchi.

"Jengo hili limekaa karibu mwaka sasa halikamiliki. Umefika wakati muweze kumaliza jengo hili ili akina mama na watoto waanze kulitumia. Serikali imeweka sh. milioni 400 kwenye jengo hili, hivyo kuendelea kukaa hivi bila kukamilika ni kuitia hasara Serikali sababu itakosa mapato. Nawapa miezi mitatu, hadi Desemba 30 jengo hili liwe limekamilika.

Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi 'Bosnia' alihoji kama kwa miezi mitatu wataweza kukamilisha ujenzi wa jengo hilo wakati kwa sasa halmashauri inategemea makusanyo ya vyanzo vyake vya ndani ili kupata sh. milioni 194 za kukamilisha ujenzi wa jengo hilo.

"Mkuu wa Wilaya, nina wasiwasi kama kwa miezi mitatu wataweza kukamilisha jengo hili sababu fedha zao zinatokana na ukusanyaji wa mapato ya ndani. Hivyo tunataka kujiridhisha kama hilo litawezekana," alisema Shekilindi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Emmanuel Vuli alisema wamejipanga kukamilisha jengo hilo mara baada ya suala la wazabuni kukamilisha zabuni ya ujenzi huo Oktoba 4, mwaka huu. Hivyo kumuhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa ifikapo Desemba 30, 2021 watakuwa wamekamilisha.

"Pamoja na kwamba zile sh. milioni 400 zilizotolewa na Serikali zimekwisha, lakini vifaa vyote vinavyohitajika ili kukamilisha jengo hili vipo. Pia sisi kama halmashauri, tumeingiza sh. milioni 60 kwenye jengo hili ili kuona linakamilika. Tunachosubiri ni utangazaji wa zabuni Oktoba 4, mwaka huu ili kukamilisha ujenzi,"alisema Vuli.

Wakati huo huo, Lazaro akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Soko Kuu la Lushoto alisema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo anataka utekelezaji huo ufanyike kwa wakati hasa upatikanaji wa maji, huduma za afya, elimu na miundombinu ya barabara.

Ni baada ya kupokea kero mbalimbali za wananchi huku baadhi yao wakilalamikia baadhi ya huduma kucheleweshwa ikiwa Mji wa Lushoto kukosa maji ya uhakika, huku mabomba yakiwa hayatoi maji, lakini wananchi wakiendelea kutozwa bili hewa.

"Tumekuja kusimamia shughuli za wananchi ili kuona Serikali ya Awamu ya Sita ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inawatumikia wananchi. Rais, kwa Kata ya Lushoto peke yake ametoa sh. bilioni 1.6 kwa ajili ya kumaliza kero ya maji kwenye Mji wa Lushoto. Lakini kwa ajili ya Jimbo la Lushoto, ametoa sh. bilioni 4.4 kwa ajili ya miradi ya maji. Hivyo wananchi wasiwe na mashaka, kero ya maji inakwenda kuisha," alisema Lazaro.

Naye Shekilindi alisema Serikali imetoa sh. bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na changarawe, ambapo sh. bilioni 3.5 ni kwa ajili ya barabara yenye urefu wa kilomita 73 kutoka Mlalo- Ngwelo- Mlola- Makanya- Milingano- Mashewa kwa kiwango cha changarawe. Na sh. bilioni moja ni barabara kiwango cha lami kutoka njiapanda ya Hospitali ya Wilaya ya Lushoto, ambapo itapita hapo hospitali hadi Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, na sh. milioni 500 zitasaidia maeneo korofi ikiwemo barabara ya Dochi- Mombo ya kilomita 16, ambapo kumetengwa fungu la kutengeneza kilomita sita ikiwa ni pamoja na kuweka karavati," alisema.

Shekilindi alisema, pia Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni moja kwa ajili ya kuiendeleza Shule ya Sekondari Shambalai ambayo ni kongwe. Katika fedha hizo, sh. milioni 788.5 zitatumika kujenga miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ikiwemo madarasa manne (4), matundu sita ya vyoo, nyumba mbili za walimu na mabweni mawili. Fedha hizo ziliingia kwenye akaunti ya shule Septemba 8, 2021.

Mradi mwingine ni wa sh. milioni 213.2 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 12 ya vyoo, madarasa mawili na mabweni mawili. Hadi sasa matundu 12 ya vyoo ujenzi upo hatua ya usafi, madarasa hatua ya jamvi na mabweni hatua ya uchimbaji msingi. Na mradi wa tatu ni wa sh. milioni 30 wa umaliziaji wa maabara moja ya kemia.
Na Yusuph Mussa, Lushoto

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments