Recent-Post

Dhahabu ya mamilioni yatoweka Geita

Wafanyakazi kadhaa wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) wanashikiliwa kwa mahojiano kwa tuhuma za wizi wa madini na kuisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.

 Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa wafanyakazi hao wanashikiliwa kwa zaidi ya wiki mbili sasa tangu walipotiwa mbaroni na kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Wizara ya Madini.

Kikosi kazi hicho kinachoundwa na maofisa kutoka Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara na watumishi wengine kutoka taasisi na idara mbalimbali za Serikali kinafanya kazi kwa kujitegemea na kinaripoti moja kwa moja wizarani.

Akizungumzia suala hilo kwa tahadhari juzi, Waziri wa Madini, Doto Biteko aliithibitishia Mwananchi kushikiliwa kwa wafanyakazi wa GGM ambao hata hivyo, hakuwa tayari kuwataja majina wala idadi yao.

“Ni kweli wafanyakazi kadhaa wa GGM wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na upotevu wa madini yenye thamani ya mamilioni ya fedha na hivyo kuusababishia hasara mgodi huo pamoja na Serikali pia,” alisema Waziri Biteko

Aliongeza: “Serikali tumeingilia kati suala hili kwa sababu hadi sasa haijulikani madini hayo yaliuzwa wapi; hakuna kumbukumbu ya mauzo na huu ni uhujumu wa mapato ya umma.”

Waziri Biteko alisema uchunguzi wa suala hilo unakaribia kukamilika na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia kesho.

Kutokana na unyeti wa suala hilo, uchunguzi huo na taarifa zote za kikosi kazi hicho zimefanywa siri kiasi kwamba, hata uongozi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita haukushirikishwa kuanzia wakati wa kukamata, kuhifadhi na kusafirisha watuhumiwa.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe alisema japo ni kweli wafanyakazi hao wa GGM wanashikiliwa, lakini suala hilo liko nje ya uwezo wake kulizungumzia kwa sababu linashughulikiwa na mamlaka nyingine.

“Ninachokuthibitishia ni kweli kuna wafanyakazi kadhaa wa GGM wanahojiwa, lakini kazi hiyo inafanywa na kikosi kazi maalumu, haliko mikononi mwetu ndiyo maana hata hawakuhifadhiwa kwenye mahabusu yoyote ya Polisi Geita,” alisema Kamanda Mwaibambe.

Maelezo kama hayo pia yalitolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Yahaya Samamba aliyeiambia Mwananchi kuwa licha ya suala hilo kuhusu madini, Tume hiyo haiwezi kulizungumzia kwa sababu kikosi kazi maalumu kinachowahoji watuhumiwa hao kimeundwa na kuripoti moja kwa moja wizarani.

“Kweli suala linalochunguzwa linahusu madini na moja kwa moja linahusu Tume ya Madini, lakini kwa uhakika sisi Tume ya Madini hatuwezi kulizungumzia kwa sababu kikosi kazi kile kimeundwa na Wizara ambayo pia ndiyo inayopokea taarifa. Nakushauri uwasiliane na viongozi wa Wizara ya Madini,” alisema Samamba.

Habari za uhakika zilizoifikia Mwananchi zinaonyesha kuwa Kikosi kazi maalumu cha Wizara ya Madini siyo tu kinafanya uchunguzi katika mgodi wa GGM, bali pia katika maeneo na migodi mbalimbali nchini; nia ni kuhakikisha mapato halali ya Serikali kupitia sekta ya madini yanakusanywa.


Mkakati wa Serikali

Serikali inatekeleza sera na mikakati kadhaa kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya madini, ikiwemo ujenzi wa masoko ya kununua na kuuza madini katika mikoa yote ya Tanzania Bara kuongeza usimamizi na udhibiti wa biashara ya madini.

Udhibiti huo tayari umeanza kuzaa matunda baada ya mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa kuongezeka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2015 hadi asilimia 6.7 mwaka 2021.

Akizungumza na Mwananchi wakati wa moja ya ziara zake mkoani Mwanza, Waziri Biteko alitaja siri ya kuongezeka kwa pato la Taifa kupitia sekta ya madini kuwa ni udhibiti, usimamizi makini, utekelezaji wa sera na sheria ya madini, ujenzi wa viwanda vya kuchenjua madini na ongezeko la shughuli za madini nchini.

“Wizara imeweza kukusanya zaidi ya Sh544 bilioni, sawa na asilimia 103 ya malengo ya kukusanya Sh526 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2020/21. “Ni malengo yetu kuwa tutakusanya zaidi ya Sh650 bilioni kwa mwaka wa fedha ujao 2021/22,” alisema Waziri Biteko.

Alisema Serikali imejiwekea malengo ya kuhakikisha sekta inachangia asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

                Na Mwandishi  Mwanza/Geita. 

Post a Comment

0 Comments