Recent-Post

DKT. SENGATI AWATAHADHARISHA WACHIMBAJI KUZINGATIA USALAMA WA WATU KABLA YA KUINGIA KATIKA MADUALA NDANI YA MGODI

 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Philemon Sengati amewataka wachimbaji wadogo wa mgodi wa Nyandorwa ulioko Solwa Wilaya ya Shinyanga kutambua kuwa wakati wanatafuta kukuza uchumi kupitia biashara na uchimbaji madini ya dhahabu ni lazima kuhakikisha usalama wa watu unazingatiwa kwa asilimia miamoja.


Dkt Sengati amsema hayo leo alipofika katika mgodi huo kujionea zoezi la kuwakwamua watu walionasa katika duara namba nne ambalo kwa siku mbili zilizopita liliporomoka na kufukia baadhi ya wachimbaji mgodini hapo na kusifu juhudi ambazo zimefanyika kunusuru maisha ya wachimbaji sita waliokuwa wamenasa katika kifusi hicho.

Aidha Dkt. Sengati aliwapongeza wachimbaji kwa juhudi zao za kuendelea kuchimba udongo katika eneo la ajali kwa lengo la kutaka kujiridhisha kama bado kuna mtu ambaye bado amenasa katika duara hilo.

Mkuu wa Mkoa aliwakumbusha kuwa watu hao ni watanzania na ni rasimali mali muhimu ambayo bado inahitajika na kwamba bila watu hawa rasilimali ya madini haiwezi kusaidia katika kutumia utajiri huu tuliojaliwa na Mungu na kuwataka kuendelea kijiridhisha ili hatimaye waweze kuona kama kuna aliyebaki chini ya duara na kuendelea na kazi za kukuza uchumi.

‘’Ndugu zangu haya yaliyojitokeza yakawe shamba darasa tufanye tahimini ya haya yaliyojitokeza na tukague maeneo yetu ili kubaini kama kuna dalili za kudondoka kama ilivyotokea hapa na kuyawekea alama za hatari.’’Aliendelea kusisitiza Dr. Sengati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Awali mchimbaji mdogo aliyenasuriwa katika kifusi cha duara hilo Toga Lukaga mkazi wa Malinyi Mkoani Morogoro aliimbia kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Shinyanga ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuwa ajali hiyo ilitokea tare 15 mwezi huu wakati yeye na wenzake watano walipozama katika duara hilo kwa ajili ya kuanza kazi.

Bw. Lukaga alibainisha kuwa wakiwa ndani ya duara walibaini kuwepo kwa nyufa katika dura hilo ndipo alipowaambia wanzake kwamba waondoke katika eneo hilo lakini wakiwa bado wanatafakari ndipo duara hilo lilipoanza kuporomoka.

Lukaga aliendelea kusema kuwa yeye na wenzake watatu walibahatika kujinisuru na kati yao wawili walibanwa na kifusi na mmoja kukatika mguu na mwingine mkono na kuongeza kuwa mfanyakazi mwenzao aitwaye Burugu Clement hawajafanikiwa kumuona mpaka sasa kwani katika harakati za kujiokoa alikimbilia katika njia yake tofauti na wao.

Naye Bw. Abubakary Magesa ambaye kwa vyeo vya uongozi wa Mgodi ni Inspekta alisema pamoja na wafanyakazi waliokuwa wanafanyakazi chini ya duara inspekta wenzake watatu waliofika eneo la hilo duara kuangalia kilichokuwa kinaendelea ili kutoa msaada nao waloporomoka pamoja na kifusi lakini waliokolewa na kufanya idadi ya waliookolewa kuwa sita.

Aidha Frank Bundala ambaye pia ni kiongozi katika mgodi huo aliongeza kuwa awali kazi ya uokozi ilikuwa ngumu kutoka na uwepo wa kifusi kikubwa lakini baada ya kutumia gereda kutoa kifusi hicho sasa wamepata njia ya kuendelea chini zaidi ili waweze kujilidhisha kuona kama kuna mtu yeyote ambaye bado amenasa chini ya duara hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko aliutaka uongozi wa mgodi huo kuhakikisha wanakuwa na takwimu sahihi za watu watakao kuwa wanaingia ndani ya duara kwa ajili ya kuchimba madini ili kuondoa sintofahamu au kuwa na idadi sahihi na majina wakati tatizo kama hili litakapojitokeza katika siku za usoni.

Wachimbaji hao wanaendelea kuchimba eneo hilo na kutafuta njia nyingine zinazoingiliana na duara hilo chini kwa chini ili kubaini kama bado kuna aliyekwama katika duara ili na baada ya zoezi hilo kukamilika wataendelea na shughuli zao kama kawaida.

  Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Philemon Sengati akipunga Mkono kuongea  wachimbaji wadogo wa mgodi wa Nyandolwa ulioko Solwa Wilaya ya Shinyanga jana alipofika katika mgodi huo kuwapa pole kufuatia kuporomoka kwa duara namba nne la mgodi huo

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Philemon Sengati akiongoza kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa kuelekea eneo la lilipo duara namba nne lililoporomoka nakujionea zoezi la uokozi linavyoendelea kujiridhisha kama bado kuna watu waliokwama ndani ya duara hilo.

Mwonekano wa duara namba nne baada ya wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Nyandolwa kutoa kifusi na kuendelea na zoezi la uokoaji watu baada ya duara namba nne kuporomoka.

 Baadhi ya wachimbaji wadogo wa mgodi wa Nyandolwa ulioko Solwa Wilaya ya Shinyanga wakifuatilia jambo wakati kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa alipofika katika mgodi huo kuwapa pole kufuatia kuporomoka kwa duara namba nne la mgodi huo.

 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt Philemon Sengati akipunga Mkono kuongea wachimbaji wadogo wa mgodi wa Nyandolwa ulioko Solwa Wilaya ya Shinyanga jana alipofika katika mgodi huo kuwapa pole kufuatia kuporomoka kwa duara namba nne la mgodi huo.

                             Na Anthony Ishengoma-Shinyanga

 

Post a Comment

0 Comments