Recent-Post

Fedha, vyeo chanzo cha migogoro ya dini

Serikali imesema kuna changamoto ya migogoro ya viongozi wa taasisi za dini inayosababishwa na fedha na vyeo kwenye maeneo ya ibada.

Migogoro hiyo imetajwa kuwa ni chanzo cha viongozi haohao kutumia madhabahu kama kijiwe cha kusutana, mipasho, kujidai, kutamba na kutoa matamko yasiyokuwemo kwenye Biblia.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene wakati akizungumza katika ibada ya kusimika maaskofu watatu wa Makanisa ya Pentekoste Renewal Assembly, iliyofanyika kwenye makao makuu ya kanisa hilo jijini hapa.

Alisema viongozi wengi wa dini wanaabudu kwa namna wanavyotaka wao na sio matakwa ya Mungu, ndiyo chanzo cha ugomvi miongoni mwao.

“Iko migogoro ambayo kwa kweli inasikitisha, imefika hatua nasuluhisha migogoro ofisini kwangu mpaka natoa machozi mbele ya maaskofu wawili wanaogombana, mpaka nikapiga magoti kuwaomba waache migogoro kwa sababu inawagawa waumini wao,” alisema Simbachawene na kuongeza:

“Lakini maaskofu hao wanakwambia haiwezekani, mpaka natoa machozi wanakwambia haiwezekani, tunatoka kwenye kikao tunaingia ofisini nawaweka wawili nawalilia lakini hawasikii, migogoro ipo palepale,” alisema.

Kwa upande wake, Askofu mkuu wa kanisa la Pentecoste Renewal Assembly, Willson Mwaoga aliwataka maaskofu waliosimikwa kuepuka migogoro baina yao na viongozi wengine wa makanisa, kwani hali hiyo inagawa waumini wao.

Aliwataka maaskofu hao wakawe chachu ya kuondoa migogoro hiyo ambayo inatokana na kugombania madaraka na fedha.

Pia, aliwataka kwenda kuleta umoja na mshikamano kwenye maeneo yao na kuanzisha taasisi mbalimbali ili kuwasaidia vijana na kuendeleza kuhubiri neno la Mungu.

Naye Katibu mkuu wa kanisa hilo, Dk Baraka Mwandikwa aliiomba Serikali kuwa changamoto zote za kidini zishughulikiwe na mabaraza husika badala ya kwenda serikalini moja kwa moja.

“Tunapenda kuchukua fursa hii kuiomba Serikali kwamba changamoto zote za kidini zishughulikiwe na mabaraza ya kidini badala ya kwenda serikalini, hilo litafanyika iwapo yameshindikana kutatuliwa huko,” alisema Dk Mwandikwa.

                                                   Dodoma. 

Post a Comment

0 Comments