Hapa kuna vita nzito!

 

NAMBA hazidanganyi hata kidogo! Angalia kikosi kipya cha Simba, kisha angalia maingizo mapya katika eneo la mbele ndio utajua Msimbazi msimu huu wamepania maradufu.

Pengine hujaelewa kitu. Simba na Yanga zimefanya usajili wa aina yake kwenye vikosi vyao vya kuimarisha eneo la ushambuliaji, kila upande ukibeba majembe ya maana, huku pia zikihamwa na wachezaji wake kadhaa waliokuwa nyota kwa msimu uliopita.

Simba iliyomaliza msimu huo ikiwa mabingwa kwa msimu wa nne mfululizo na kufunga jumla ya mabao 78, imepoteza nyota wawili tu waliochangia mabao hayo, Luis Miquissone na Clatous Chama waliouzwa kwa Al Ahly ya Misri na RS Berkane ya Morocco.

Luis alioyefunga mabao 9 ameuzwa Al Alhy na Chama yeye alienda Morocco akiwa na mabao nane, lakini wawili hao wakishirikiana kutengeneza jumla ya mabao zaisi ya 20, ikiwa na maana Simba imetema jumla ya mabao 17 na asisti za maana ndani ya kikosi chao cha sasa.

Hata hivyo, Simba imesajili washambuliaji watano ambao wote katika klabu zao walizotoka wakifunga mabao 32, ikiwa ni karibu mara mbili ya mabao iliyopoteza kwa kuondoka kwa Luis na Chama.

Simba imevuta Kibu Denis (Mbeya City), alimaliza msimu uliopita na mabao saba, Pape Ousmane Sakho (Teungueth Rufisque) aliyefunga mabao nane na Yusuph Mhilu (Kagera Sugar) aliyetupia mabao tisa, Peter Banda (Sheriff Tiraspol) mabao sita na Jimsony Mwanuke aliyetokea Gwambina aliyemaliza msimu uliopita na mabao manne na timu yake hiyo ya zamani ikishuka daraja.

BALAA LIPO HAPA

Wakati Simba ikisajili jumla ya mabao 32, lakini kikosi pia ina wakali watano wa mabao waliobakishwa akiwamo John Bocco, Chriss Mugalu, Meddie Kagere, Hassan Dilunga na Ibrahim Ajibu ambao wote wamefunga jumla ya mabao 46, ikiwa ni zaidi ya nusu ya mabao ya msimu mzima wa timu yao ya Simba.

Nahodha Bocco, ndiye aliyekuwa kinara wa ufungaji msimu uliopita kwa kufunga mabao 16, Mugalu aliyemaliza wa pili na mabao 15, huku Kagere akifunga 13 wakati Dilunga na Ajibu kila mmoja alifunga mawili.

Kutokana na kupata mabadala sahihi wa Luis na Chama na hao waliobaki, wapinzani wao namba mmoja nchini Yanga huenda wakasubiri sana kutokana na rekodi ya kikosi chao zilivyo, kwani kwa hesabu za haraka mpaka sasa ni kwamba Simba imekusanya mabao ya kutosha hata kabla msimu haujaanza.


YANGA SASA

Rekodi kwa upande wa Yanga zinaonyesha wamewaacha wachezaji watano ambao msimu mzima wote wamefunga mabao 14, ikiwa sawa na theluthi ya mabao yao 52 iliyofungwa na timu hiyo kwa msimu mzima.

Walioachwa ni Michael Sarpong aliyefunga manne, Tuisila Kisinda (5), Carlos Carlinhos matatu, Waziri Junior na Haruna Niyonzima kila mmoja alifunga bao moja.

Yanga imefanya usajili wa washambuliaji wanne ambao wote wamefunga mabao 22, ambao ni Fiston Mayele, Heritier Makambo, Jesus Moloko na Dickson Ambundo kutoka Dodoma Jiji Fc.

vita pcc

Rekodi zinaonyesha Mayele aliyemaliza msimu na AS Vita amefunga mabao 13, Moloko mabao mawili, Makambo mabao matatu na hakuwa anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza cha AC Horoya ya Guinea huku Ambundo alimaliza na mabao manne.

Wakati huo huo, Yanga imewabakiza washambuliaji wao watano ambao rekodi zao za kufunga msimu uliopita haziwabebi ambao ni, Yacouba Songne, Saido Ntibazonkiza, Deus Kaseke, Farid Mussa na Ditram Nchimbi na wakati mwingine kubebwa na kiungo aliyekuwa akichezeshwa kama mshambuliaji namba mbili, yaani Feisal Salum ‘Feitoto’ aliyefunga mabao matano msimu uliopita.

Msimu uliopita Yacouba ndio aliibuka kinara wa ufungaji akiwa na mabao nane, huku Kaseke akifuata na mabao sita, Feisal (mabao matano), Saido (mabao manne) huku Farid na Nchimbi kila mmoja alifunga bao moja hili nalo linaonyesha kiasi gani safu hiyo ya Yanga msimu uliopita ilikuwa na uhaba.

Kutokana na rekodi za wachezaji waliondoka msimu uliopita, waliobaki msimu na wale ambao wamesajiliwa namba zinawabana katika kufunga tofauti na ilivyo kwa wapinzani wao Simba.

WASIKIE HAW

Kocha wa zamani wa Simba, Masoud Djuma anasema jambo kubwa ambalo timu hiyo imefanya ni kubakisha wachezaji wake muhimu wa safu ya ushambuliaji.

Anasema Simba kupoteza wachezaji wawili kama Luis na Chama lazima kuna mahali watatikisika lakini kama kuziba yote hayo hao wapya waliosajiliwa wanatakiwa kufanya vitu bora zaidi.

Yanga ambacho wanahitaji msimu ujao ni kufanya vizuri na si jambo lingine lolote kwa hiyo hao wachezaji ambao wamewasajili huenda rekodi zikawa zinawabana, lakini wakaja kuonyesha viwango bora,” anasema Djuma.

Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kiwelo ‘Julio’ anasema kama kocha wa Yanga atatuliza kichwa chake vizuri kikosi hicho kinaweza kuwa na timu nzuri kwa sababu wanakosa tu muunganiko.

Kama wataweza kutengeneza muunganiko na maelewano kwa wachezaji waliokuwepo msimu uliopita na awamu hii watakwenda kuleta ushindani wa kutosha dhidi ya wapinzani wao Simba si katika kufunga tu bali kwenye maeneo yote, naamini msimu ujao kutakuwa na vita nzito kwelikweli,” anasema Julio.

Kocha wa zamani wa Yanga, Mwinyi Zahera, naye alisema kwa aina ya wachezaji waliosajiliwa Jangwani kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa ushindani mkali kuliko wa misimu minne iliyopita, kwani majembe yaliyoingia yataenda kuiongezea makali safu ya mbele, huku Simba nayo sio wa kubezwa hata kidogo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments