Recent-Post

Haya Ndiyo Madhara Ya Pombe Kiafya, Kijamii

Matumizi ya pombe kupita kiasi ni moja ya vichocheo vya magonjwa yasiyoambukiza, anaeleza Dk Omary Ubuguyu, meneja mpango wa Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya.

Mtaalamu huyo anaeleza hata kiwango cha pombe kinachofaa kwa matumizi.

“Mwanamke asizidishe bia moja kwa siku na mwanaume asizidishe bia mbili kwa siku. Wanawake wengi wanapenda mvinyo au wine, anatakiwa anywe mililita 125 za wine sawa na glass kwa siku usizidishe na wanaume 250,” alisema.

Dk Ubuguyu alisema ili viungo vya mwili viweze kuchakata sukari vizuri na taka zote zitokanazo na pombe katika viwango, kwa wiki mwanaume asizidishe uniti 14 na mwanamke uniti saba. Uniti moja ni sawa na asilimia 4 ya kilevi.

Alisema kwa ujumla pombe inaathiri mfumo wote wa mwili kuanzia utumbo ambapo husababisha vidonda vya tumbo hasa inapoingia katika mfumo wa usafishaji mwili.

“(Pombe) Inaweza ikawa kama kichocheo cha mazingira, saratani ya koo na kutapika na ukali wa pombe unachoma tezi kongosho ambayo inatoa insulin inayosaidia kusaga sukari na usagaji wa sukari ukiathirika kinachotokea mtu anapata ugonjwa wa kisukari,” alisema.

Dk Ubuguyu alifafanua kuwa pombe inaathiri ubongo na mara nyingi watu hupoteza kumbukumbu wanapozitumia.

“Kwenye ubongo pombe huondoa baadhi ya madini,hasa folic acid, na ikipungua inaathiri ubongo na kupoteza kumbukumbu,” alisema.

Alizitaja pombe kali za asili kama gongo, kuwa ina taka sumu nyingi ambazo mwili wa binadamu hauhimili na ndiyo maana ni haramu.


Husababisha migogoro

Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Kinondoni, Judith Kimaro alisema, “madhara ya pombe ni makubwa na wamesuluhisha migogoro 266 iliyosababishwa na pombe.

Vilevile, alisema pombe imesababisha watoto kuwa yatima kutokana na vifo ambavyo vinaweza kutokea.”

Kwa mujibu wa Kimaro, manispaa hiyo inaongoza kwa kuwa na baa nyingi kuliko wilaya zingine nchini huku, huku ikiwa na migogoro 1,134 ya ndoa na mahusiano inayosababishwa na matumizi ya pombe.

Alisema manispaa hiyo ambayo imesajili baa 2,069 kati ya 2016/2017 imesuluhisha kesi 76 za pombe na kumekuwa na kesi 40 mahakamani zinazotokana na ubakaji na ukatili wa kijinsia kutokana na matumizi ya pombe. Alisema kutokana na tatizo hilo manispaa hiyo ina migogoro ya familia ambayo inaendelea kusuluhishwa 765 huku familia 27 zikiwa zimesambaratika mwaka 2016/2017.

Alishauri Serikali kutoa elimu, kuweka mitalaa ya madhara ya pombe kwenye elimu ngazi ya msingi na hadi vyuo na kuweka kipaumbele katika mapambano dhidi ya pombe kama ambavyo imeweka katika maambukizi ya malaria na virusi vya Ukimwi.


Chanzo cha ajali nyingi

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa alisema mojawapo ya uvunjifu wa sheria za barabarani kwa waendesha madereva ni pamoja na ulevi.

Mwaka 2017 mwanasheria wa kikosi hicho, Deus Sokoni alisema jumla ya ajali 2,250 zilitokea kati ya 2006 na 2017 nchini kutokana na ulevi.

Hii inamaana kila baada ya siku mbili ajali moja inayohusisha ulevi ilitokea.

Mwaka 2018 jumla ya ajali 61 zilisababishwa na ulevi, hii ni ilimaanisha ajali moja kati ya 61 zilizotokea mwaka huo zilisababisha na tatizo hilo huku mwaka 2019 ajali moja kati ya 59 ilitokea ikiashiria kuongezeka kwa ajali zitokanazo na ulevi.

Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dk Athuman Ngenya alisema mamlaka hiyo hufanya ukaguzi wa kushtukiza masokoni na mipaka isiyo rasmi pale inapogundulika uwepo pombe haramu kuinmgizwa nchini.

Imeandikwa na Elias Msuya, Herieth Makweta, Elizabeth Edward.

Post a Comment

0 Comments